Tuesday, April 13, 2010

IBADA YA NDOA

Ibada ya ndoa ifuatayo ni matokeo ya maswali aliyoniuliza kijana mmoja yalitosema; "Kwa nini ibada ya upadre na ndoa ni tofauti sana? Ibada ya ndoa ni fupi sana na ile ya upadre ni ndefu na ina mambo mengi kuliko ya ndoa ambayo ni wito mama wa miito yote. Tena wakati wa ibada ya ndoa wanaoshiriki ibada hiyo kanisani ni wachache sana ukilinganisha na idadi ya wale wanaoshiriki kwenye ukumbini. Vile vile, shamra shamra ukumbini ni za hali ya juu na utaratibu wa yale yanayotokea ukumbini ni moto moto, lakini kanisani watu huwa baridi sana, tena wazazi, hawana nafasi maalumu kanisani.


Kutokana na hayo imenibidi kufanya utafiti ili tuweze kuwa na ibada ya ndoa ambayo kweli itawafanya bwana na bibi harusi waweze kuzama kwenye tukio hilo muhimu na nafasi mbali mbali kwa wazazi, waamini, na wasimamizi pamoja na alama mbalimbali ambazo zinaweza kuwazamisha bwana na bibi harusi kuelewa vema fumbo la ndoa takatifu.


Nakaribisha maoni mbalimbali kuhusu ibada hii ambayo ni matokeo ya utafiti nilioufanya nikiwa katika Chuo cha Kichungaji Eldoret.



IBADA YA NDOA

Maandamano:
Wakati wa maandamano utaratibu utakuwa kama ifuatavyo:-
· Watumishi wenye kubeba chetezo na ubani
· Mtumishi mwenye kubeba Msalaba
· Bi harusi akiwa katikati ya wazazi wake; (mama upande wa kushoto na baba upande wa kulia)
· Waimbaji
· Bwana harusi akiwa katikati ya wazazi wake; (mama upande wa kushoto na baba upande wa kulia.)
· Wasimamizi
· Watumishi
· Mapadre

Bwana na Bi harusi wakiingia kanisani, Bi harusi atakaa nyuma ya Kanisa upande wa kushoto wa Kanisa akiwa katikati ya wazazi wake na Bwana harusi atakaa nyuma ya kanisa upande wa kulia wa kanisa akiwa katikati ya wazazi wake. Wasimamizi wanaweza kukaa pamoja popote kati ya waamini.

Baada ya kila mtu kuchukua nafasi yake, Padre anawakariBisha waamini kwa maneno yafuatayo:

Maneno ya Mwanzo
P. Tumekusanyika hapa mbele ya MUNGU kama rafiki, ndugu na jamaa kushuhudia ndoa ya (F) na (F) kumwomba MUNGU ili awabariki. Imeandikwa: “MUNGU asipoijenga nyumba waijengao wanajisumbua bure.” Tena imeandikwa: "Katika njia zako mkubali MUNGU na atazinyoosha njia zako.” (F) na (F) mmeonesha nia yenu ya kuingia kwenye hali ya ndoa takatifu na hakuna yeyote aliyeonesha kwamba hamstahili.

Sala ya Mwanzo
P. Tuombe:
BABA wa Mbinguni, tunakuomba baraka zako juu ya (F) na (F) wanapokuja mbele yako sasa na kuweka maagano yao ili wawe kitu kimoja maisha yao yote. Uwaimarishe kwa zawadi ya ROHO MTAKATIFU, ili daima wawe wakweli na wanaopendana. Chapa mioyo yao kwa uelewano na msamaha. Nyumba yao iwe mahali pa upendo na wema, ambapo hakuna atakayejisikia mgeni. Uwalinde na daima uwaweke chini ya ulinzi wako unapotembea pamoja nao katika maisha yao. Uwakinge kwa neno lako na wakutumikie wewe katika maisha yao yote. Tunaomba hayo kwa njia BWANA wetu YESU KRISTO mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika ROHO MTAKATIFU MUNGU, daima na milele. Amina.

Kuitwa kwa wasimamizi, bwana harusi na wazazi wake, Bi harusi na wazazi wake.

Kabla ya Liturujia ya Neno, Padre anawaita wasimamizi, bwana harusi na wazazi wake, bi harusi na wazazi wake kama ifuatavyo:

P. Wale ambao ni wasimamizi wa ndoa hii wajongee mbele.

Wasimamizi wanasimama na kujongea mbele huku wakishangiliwa, watapeana mikono na padre kisha watakaa upande wa kulia wa Padre wakiwaelekea waamini. Kisha Padre anamwita bi harusi.

P. Bi harusi ajongee mbele.

Bi harusi anajongea mbele huku akisindikizwa na wazazi wake. Wakifika mbele, padre anawapokea bi harusi na wazazi wake kwa kuwashika mkono na kuwaelekeza kusimama upande kushoto wa Padre. Anafanya hivyo hivyo kwa kumuita bwana harusi. Wote wakifika mbele watakuwa wanatazamana huku bwana harusi akiwa kati kati ya wazazi wake, hali kadhalika, bi harusi huku wakiwa wanatazamani wakiwa umbali wa kama mita tatu hivi. Wakati wazazi wakiwasindikiza watoto wao, mmoja wao atakuwa ameshika mshumaa huku wakisindikizwa kwa muziki wa ala, na waamini wakishangilia na kupiga makofi.

Uthibitisho wa wazazi juu ya nia ya bwana na bi harusi

Kisha baba wa bwana harusi anamhoji mototo wao kwa maneno yafuatayo:

Baba: Mwanetu, je, huyu ndiye msichana uliyemchagua kuwa mkeo?

Bwa. harusi: Ndiyo, wazazi wangu, ni yeye kabisa.

Baba: Je, uko tayari kumpenda, kumtegemeza na kumtunza kwa maisha yote?

Bwa. harusi: Ndiyo, wazazi wangu, niko tayari.

Baba: Itakuwaje endapo atakuwa kipofu, au kiziwi au kilema?

Bwa. harusi: Nitamwongoza.

Baba: Itakuwaje endapo uso wake utaharibika na kushindwa kujimudu?

Bwa. harusi: Nitazidi kumpenda, kumtunza na kuishi naye.

Mama: Mwanetu, kama ni hivyo unavyotaka, achana sasa na hali ya utoto kwani u mtu mzima sasa. Uende kuwajibika kwa mke wako na familia yako. Nenda kawe mume bora na dhihirisha ubaba wako katika ndoa yako. Usituangushe sisi wazazi wako. MUNGU akubariki mwanetu.

Kisha wazazi wanamkumbatia bwana harusi na kumtakia kila la heri kwa maisha ya ndoa yake, huku watu wakishangilia. Kisha wazazi wa bi Harusi wanamhoji binti yao:-

Baba: Binti yetu mpendwa, ni vema kwamba tunakutoa katika ndoa takatifu; kwani wasichana wanatarajiwa kuacha wazazi kwa ajili ya ndoa takatifu na kuwapa fahari wazazi wao. Je, huyu ndiye kijana uliyemchagua kuwa mume wako?

Bi Harusi: Ndiyo, wazazi wangu ni yeye kabisa.

Baba: Je, uko tayari kumpenda, kumtegemeza na kumtunza kwa maisha yako yote?

Bi Harusi: Ndiyo, wazazi wangu, niko tayari.

Baba: Itakuwaje endapo atakuwa kipofu, au kiziwi au kilema?

Bi Harusi: Nitamwongoza.

Baba: Itakuwaje endapo uso wake utaharibika na kushindwa kujimudu?

Bi Harusi: Nitazidi kumpenda, kumtunza na kuishi naye.

Mama: Binti yetu mpendwa, ikiwa ni hivyo, onyesha kuwa u mke bora na mfano katika ndoa yako na mama kwa watoto wako. Mpende mumeo na heshima kwa watu wake. Kuwa mkarimu na shirikisha chakula chako na wote.

Baraka na kumtoa Binti kwa Bwana harusi

Baba: Mama yako na mimi tunakutoa kwa mumeo. Nenda na baraka zetu mwanetu na MUGNU akubariki.

Wazazi wanamtemea mate kidogo kwenye mikono na mama anamtemea kwenye matiti huku akisema maneno yafuatayo wakati mkono wake wa kulia umegusa tumbola Binti yake.

Mama: Tumbo lako liwe na uzao na matiti yako yatoe maziwa. Upendwe na upokelewe vema na mumeo na watu wake. Nenda na amani mwanetu.

Kisha wazazi wa bi harusi wanamkabidhi mototo wao kwa bwana harusi akiwa pamoja na wazazi wake huku watu wakishangilia na wimbo ufaao kuimbwa. Bwana harusi na wazazi wkea wanampokea bi harusi pamoja na wazazi wake. Baada ya tendo hilo, bwana na bi harusi wakiwa na wasimamizi wao wanakaa katika sehemu ilioyoandaliwa, hali kadhalika wazazi wa pande zote mbili wanakaa pamoja sehemu iliyoandaliwa. Kisha padre anasema maneno yafuatayo:-

P. Bwana harusi na bi harusi, kanisa linashiriki furaha yenu na linawapokea kwa moyo mkunjufu pamoja na wazazi na rafiki zenu katika siku ambayo, mbele ya Baba MUNGU wetu, mmeamua kuunda umoja wa ndani kati yenu. Bwana apende kuwasikiliza katika siku hii ya furaha kwenu. Awapelekee msaada kutoka mbinguni na kuwalinda. Awajalie mema yote kulingana na moyo wenu na asilize dua zenu zote.

Akiwaelekea wazazi, padre anasema;

P. Nanyi wazazi wapendwa, Kanisa linawapa pongezi kwa malezi yenu mazuri mkishirikiana na MUNGU katika kuwalea kwa maneno na mifano yenu bora watoto wenu (F) na (F) hadi leo mnapowakabidhi kwa MUNGU ili kwa njia ya Sakramenti ya ndoa awaunganishe wawe mwili mmoja na roho moja kwa njia ya Sakramenti ya ndoa, na mwisho wamfikie Muumba wao pamoja na watoto watakaojaliwa na MUNGU. Hongereni sana wazazi.

Padre anawaalika waamini kuwapongeza wazazikwa kuwapigia makofi.

Kuwasha mishumaa ya familia

Baada ya maneno hayo, wazazi wa Bwana harusi wanaenda kwenye meza iliyoandaliwa na kuwasha mshumaa wa familia kumaanisha kwamba, wazazi wakishirikiana na MUNGU wamemleta bwana harusi duniani. Mshumaa huo ni ishara ya uhai wa bwana harusi. Kisha wazazi wa bi harusi nao wanafika kwenye meza iliyoandaliwa na kuwasha mshumaa wa familia kumaanisha kwamba, wazazi wakishirikiana na MUNGU wamemleta bi harusi duniani. Mshumaa huo ni ishara ya uhai wa bi harusi . Wakati mishumaa ikiwashwa wanakwaya waweza kuimba wimbo ufao wa mwanga. Mishumaa hiyo inaashiria pia kwamba bwana harusi na bi harusi hawajawa mwili mmoja. Baada ya tendo hili kukamilika, yanafuata masomo.

Liturjia ya Neno

Somo la Kwanza: ToBi 8:4b-8 (simtwai kwa tamaa)

Somo la Pili: Efe. 5: 2a, 25-32 (Siri hii ni kubwa; Mimi lakini naongea kuhusu KRISTO na Kanisa.)

Injili: Mt.19:3-6 (Aliyoyaunganisha MUNGU mwanadamu asiyatenganishe.)

Baada ya Injili, yanafuata mahubiri.

Ibada ya ndoa

Baada ya mahubiri, wote wanapiga magoti na padre anasali sala ifuatayo:


P. Tuombe:
MUNGU Mwenyezi, tunakuomba Baraka zako kwa (F) na (F) ambao sasa wanajiandaa kuweka maagano yao ya ndoa takatifu. Walete karibu yako na uwasaidie wakue pamoja katika upendo na kujitoa kabisa kati yao tangu sasa na milele yote. ROHO MTAKATIFU awe juu yao, wanapojifungamanisha katika maagano ya upendo na utimilifu. Tunaomba hayo kwa njia ya KRISTO BWANA wetu. Amina.


Kuwakaribisha Watakatifu wa Mbinguni

Bwana na bibi harusi wanapiga magoti mbele ya Altare huku Litania ya watakatifu ambao walikuwa wanandoa ikiimbwa au kusaliwa.

Litania ya Watakatifu

Padre anawaalika waamini kuunganika na jumuiya nzima ya Watakatifu kwa kusema:

P. Ndugu zangu, sisi ambao tupo bado duniani si wafuasi pekee wa KRISTO! Wengi wameiacha dunia hii na wako kwa MUNGU. Lakini pamoja nao, tunaunda familiya kubwa moja. Tuunganike na watakatifu, ili kwamba adhimisho hili la ndoa katika Sadaka ya Ekaristi itulete pamoja katika mwili moja.

Wote wanapiga magoti na padre anasali sala ifuatayo:

P. MARIA Mtakatifu, uwe nasi, wewe uliye MAMA wa MUNGU, uwe nasi. Hii ni sala yetu, uwe nasi, na uwe na wote wanaoadhimisha adhimisho hili.

W. Uwe nasi katika adhimisho hili, uwe nasi sote.

P. Watakatifu Yohakimu na Ana, muwe pamoja nasi, ninyi mlio wazazi watakatifu wa MARIA, muwe nasi. Hii ni sala yetu, muwe nasi, na muwe na wote wanaoadhimisha adhimisho hili.

W. Muwe nasi katika adhimisho hili, muwe nasi sote.

P. Mtakatifu Giarna Mola, uwe nasi, wewe uliye shujaa wa mpango wa uzazi kwa njia ya asili, uwe nasi. Hii ni sala yetu, muwe nasi, na muwe na wote wanaoadhimisha adhimisho hili.

W. Uwe nasi katika adhimisho hili, uwe nasi sote.

P. Wenye heri wazazi wa Mt. Teresia wa Mtoto YESU, muwe pamoja nasi, ninyi mlio wazazi wenye heri wa Mt. Teresia wa Mtoto YESU, muwe nasi. Hii ni sala yetu, muwe nasi, na muwe na wote wanaoadhimisha adhimisho hili

W. Muwe nasi katika adhimisho hili, muwe nasi sote.

P. Mt. Monika, uwe nasi, wewe uliye mzazi wa Mt. Augustino, uwe nasi. Hii ni sala yetu, uwe nasi, na uwe na wote wanaoadhimisha adhimisho hili.

W. Uwe nasi katika adhimisho hili, uwe nasi sote.

P. Mtakatifu (Somo wa Bwana harusi) uwe nasi, wewe uliye somo wa Bwana harusi uwe nasi. Hii ni sala yetu, uwe nasi, na uwe na wote wanaoadhimisha adhimisho hili.

W. Uwe nasi katika adhimisho hili, uwe nasi sote.

P. Mtakatifu (Somo wa BiBi harusi) uwe nasi, wewe uliye somo wa BiBi harusi uwe nasi. Hii ni sala yetu, uwe nasi, na uwe na wote waliopo hapa wanaoadhimisha adhimisho hili.

W. Uwe nasi katika adhimisho hili, uwe nasi sote.


Mara baada ya litania, bwana na bi harusi na wasimamizi wakiwa nyuma yao wanasimama mbele ya altare, kisha padre hutamka maneno yafuatayo:

P. Bwana harusi na bi harusi, mmefika hapa kanisani, ili mapendo yenu yapate kutiliwa muhuri mtakatifu wa BWANA mbele ya mjumbe wa Kanisa na mbele ya mashahidi wenu, wazazi wenu, rafiki zenu, ndugu na jamaa yote iliyopo hapa. KRISTO anayabariki sana mapendo hayo, na kwa Sakramenti hii ya pekee anawaneemesha kwa kuwaimarisha hao aliokwisha kuwatakasa kwa ubatizo mtakatifu kati yao na kutimiza shughuli nyingine za ndoa. Ndio maana nawahoji mbele ya Kanisa juu ya nia zenu.

Mahojiano kabla ya kukubaliana

P. (F) na (F), je, mmefika hapa kufunga ndoa pasipo shuruti, kwa hiari na kwa moyo radhi?

Kila mwanaharusi anajibu: Ndiyo.

P. Je, mko tayari kuishi maisha ya ndoa, kupendana na kuhesimiana siku zote za maisha yenu?

Kila mwanaharusi anajibu: Ndiyo.

P. Je, mko tayari kuwapokea kwa mapendo watoto mtakaopewa na MUNGU na kuwalea kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa lake?

Kila mwanaharusi anajibu: Ndiyo.


Kukubaliana

Kabla ya kukubaliana, bwana harusi anapiga magoti mbele ya altare huku msimamizi wake akiwa nyuma yake na kusali sala ifuatayo:

Bw.harusi: Ee Mwumbaji wetu, umenena: “Nyumba na mali ni urithi aupatao mtu kwa babaye; bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” Hali kadhalika, ni wewe mwenyewe unayeunganisha watu katika ndoa takatifu. Nami natarajia kwa matumaini makubwa kupokea Sakramenti hiyo muda mfupi ujao na mwenzangu (F) maisha yangu yote.

Kwa hiyo nakuomba, ee BWANA, huyu (F) uliyenichagulia kuwa mwenzi wa maisha, awe kweli ni mcha MUNGU, safi na mwaminifu. Uzuri wake uwe hasa wa roho kuliko uso, zaidi tabia njema kuliko umaridadi.

Mioyo yetu iwe ya kulingana, nia zetu zipatane, tupate kuishi maisha ya pamoja kwa amani na kuwalea watoto wetu utakaopenda kutujalia, kulingana na mapenzi yako. Siku zote tukusifu wewe MUNGU huku tukikushukuru Wewe Mpaji wa vyote.

Mama Bikira MARIA, unisimamie na uniombee kwa Mchumba wako ROHO MTAKATIFU anipe nuru yake na ushujaa wa kuiishi ndoa yangu hii, kadiri ya mapenzi ya MUNGU, nikivumilia yote yatakayojitokeza katika maisha ya ndoa yetu hadi mwisho mimi na mwenzangu (F) na watoto utakaotujalia tufike kwako mbinguni. Ninaomba hayo kwa njia ya KRISTO BWANA wetu. Amina.

Baada ya kumaliza, bi harusi naye anajongea mbele na kupiga magoti kisha naye husali sala hiyo akiwa na msimamizi wake akisimama nyuma yake huku akiwa amepiga magoti;

Kisha wote wawili wanapiga magoti kuomba nguvu na maongozi ya ROHO MTAKATIFU awaimarishe kabla ya kukubaliana. Wakiwa wamepiga magoti wimbo wa “NJOO ROHO MTAKATIFU” au wimbo wowote wa ROHO MAKATIFU, huimbwana

MAHOJIANO
Wazazi kuhojiwa

Baada ya wimbo huo, wazazi wa pande zote mbili wanaitwa mbele. Wanasimama nyuma ya watoto wao ambao wakati huo wamepiga magoti, kisha padre anawauliza.


P. (F) na (F) wanavyounganisha maisha yao katika ndoa, wanawaleta ninyi pamoja katika mahusiano mapya na ya pekee, kuanzisha muungano wa kuaminiana na vifungo vya mahusiano. Nawauliza mbele ya MUNGU, je, mtawapa upendo wenu, baraka zenu, na kuwasaidia katika maisha yao ya ndoa?

Wazazi: Ndio, kwa msaada wa MUNGU tutafanya hivyo.

Baada ya hapo wazazi wanakaa katika sehemu zao.

Wasimamizi kuhojiwa

Akiwauliza Wasimamizi:

P. Mnaposhuhudia nia ya (F) na (F) ya kufunga Ndoa Takatifu, thibitisheni kwamba mtawasaidia katika maisha yao. Je, kwa msaada wa MUNGU mtajitahidi kwa kadiri ya uwezo wenu wote kuwasaidia na kuwatunza (F) na (F) katika ndoa yao?

Wasimamizi: Kwa Msaada wa MUNGU tutawatunza.

Waamini kuhojiwa

Akiwauliza waamini wakiwa wamesisimama:

P. Ndugu zangu, ninyi mmealikwa hapa na (F) na (F) kwa sababu ni watu muhimu sana katika maisha yao. Mapendo yenu na msaada wenu kwao vitakuwa muhimu daima. Ninyi nyote kwa pamoja, kwa neema za MUNGU, fanyeni yote kwa uwezo wenu wote kutunza ndoa yao. Ninawuliza mbele ya MUNGU, je, mtawapa upendo wenu, baraka zenu, na kuwasaidia katika maisha yao?

Wote wanajibu: Ndiyo.

Kisha padre anawaalika wanaharusi waonyeshe kukubaliana kwao.

P. Basi kwa vile (F) na (F), mwakusudia kufanya maagano ya Ndoa Takatifu, shikaneni mikono ya kuuume na kuonyesha kukubaliana kwenu mbele ya MUNGU na Kanisa lake.

Wanaharusi wanashikana mikono ya kuume Bila kuachiana huku walielekeana.

Bwana harusi anasema:

Mimi (F) nakupokea wewe (F) uwe mke wangu, nikijua moyoni fika kwamba utakuwa rafiki yangu, mwenzi wangu katika maisha na mpendwa wangu wa pekee na wa kweli. Katika siku hii ya pekee, mbele ya MUNGU, ninakuahidia kuwa nawe kama mume wako, katika magonjwa na afya, katika raha na taabu, pia katika nyakati za heri na mbaya. Ninaahidi kukupenda bila kujibakiza, kukujali na kukuheshimu, kukupatia mahitaji muhimu kwa uwezo wangu wote, kukua pamoja nawe katika moyo na roho, daima nikiwa wazi na mkweli kwako na kukufurahisha pindi wote tuwapo hai. Nitakusamehe kama tunavyosamehewa, na nitajitahidi pamoja nawe kuielewa dunia, MUNGU na sisi wenyewe, kupitia mazuri na magumu tutatakayokumbana nayo hadi kifo kitutenganishe.

Bi harusi anasema:

Mimi (F) nakupokea wewe (F) uwe mume wangu, nikijua moyoni fika kwamba utakuwa rafiki yangu, mwenzi wangu katika maisha na mpendwa wangu wa pekee na wa kweli. Katika siku hii ya pekee, mbele ya MUNGU, ninakuahidia kuwa nawe kama mke wako, katika magonjwa na afya, katika raha na taabu, pia katika nyakati za heri na mbaya. Ninaahidi kukupenda bila kujibakiza, kukujali na kukuheshimu, kukupatia mahitaji muhimu kwa uwezo wangu wote, kukua pamoja nawe katika moyo na roho, daima nikiwa wazi na mkweli kwako na kukufurahisha pindi wote tuwapo hai. Nitakusamehe kama tunavyosamehewa, na nitajitahidi pamoja nawe kuielewa dunia, MUNGU na sisi wenyewe, kupitia mazuri na magumu tutatakayokumbana nayo hadi kifo kitutenganishe.

Kupokea kwa makubaliano ya wafunga ndoa

Kisha padre hupokea makubaliano ya wafunga ndoa akisema

P. Ukubaliano wenu huo mliouonyesha mbele ya Kanisa, MUNGU wa Ibrahimu, MUNGU wa Isaka, MUNGU wa Yakobo, MUNGU aliyewaunganisha watu Paradisini, authibitishe na kuubariki katika KRISTO, kusudi yale anayoyaunganisha YEYE, mwanadamu asiyatenganishe.

Kubariki na kuvishana pete

Pete za wanaharusi zinatolewa na kuwekwa kwenye kishani kilichoandaliwa, kisha padre anasemas maneno yafuatayo:

P. Tuombe:
Mduara wa pete ulio kamili unaonyesha umoja na umilele, wakati dhahabu ni alama ya vyote vilivyo safi na takatifu. Mnapovishana Pete hizi, sala yetu ni kwamba upendo wenu uwe sawa, safi na wa milele. Mzivae hizi pete kama alama ya upendo wenu kati yenu na alama ya kile mchofanya leo.

Baba wa mbinguni, uzibariki pete hizi ambazo sisi tunazibariki + kwa jina lako, kusudi hasa (F) na (F) watakaozivaa, wazivae kwa imani kubwa katika mapendo yao. watunze uaminifu kamili kati yao, wadumu katika imani wakitimiza mapenzi yako, na waishi daima pamoja, kwa amani, upendo na furaha wakipendana. Kwa njia ya KRISTO BWANA wetu.

Kisha Padre ananyunyizia pete maji ya baraka, ikifaa anafukizia pia ubani

Bwana harusi anamvika pete Bi harusi na kusema.

(F) Mke wangu, na kuvisha pete hii iwe ishara ya mapendo yangu na uaminifu wangu kwako. Pete hii, iwe pia ishara ya ndoa yetu, kwa leo na kesho, na kwa siku zote. Ivae daima pete hii kama pia alama ya kile tulichoahidi na tulichofanya leo. Kwa jina la BABA, na la MWANA, na la ROHO MTAKATIFU.

Pia, bi harusi humvika bwana harusi pete akisema:

(F) Mume wangu, na kuvisha pete hii iwe ishara ya mapendo yangu na uaminifu wangu kwako. Pete hii, iwe pia ishara ya ndoa yetu, kwa leo na kesho, na kwa siku zote. Ivae daima pete hii kama pia alama ya kile tulichoahidi na tulichofanya leo. Kwa jina la BABA, na la MWANA, na la ROHO MTAKATIFU.

Tamko la kuwa Mume na Mke

Baada ya wanaharusi kuvishana pete, wakiwa wamegeukiana na kushikana mikono, na padre kuweka mkono wake juu ya mikono ya wanaharusi, padre anatoa tamko rasmi la wanaharusi kuwa Mume na Mke halali mbele ya MUNGU na Kanisa kwa maneno yafuatayo:

P. (F) na (F) wameweka maagano yao ya ndoa mbele ya MUNGU na mbele yetu, kulingana na taratibu za Kanisa Katoliki, natamka rasmi kuwa kuanzia sasa, (F) na (F) ni Mume na Mke. MUNGU awabariki na kuwalinda, BWANA na awamiminie wingi wa baraka zake kwa kumpendeza yeye kwa mwili na roho, huku mkikua pamoja katika upendo. Kwa jina la BABA, na la MWANA, na ROHO MTAKATIFU. Amina.

Waamini wanaalikwa kushangilia.


Kuwasha Mshumaa wa Ndoa – (Wedding Candle)

P. Mishumaa hii miwili pembeni ya mshumaa mkubwa, ambayo iliwekwa na kuwashwa na wazazi wa wana harusi inawakilisha maisha ya (F) na (F). Mianga yao inaonyesha imani, hekima, na upendo waliopokea toka kwa wazazi wao, mianga iliyo tofauti na kila moja unawaka peke. Baada ya (F) na (F) kukubaliana na kuweka ahadi zao mbele ya MUNGU na mbele yetu sote, (F) na (F) watawasha mshumaa ulio katikati ya ile miwili ili kuonyesha umoja wa maisha yao kuanzia sasa na milele yote hadi kifo kitakapowatenganisha.

Hapo wanaharusi wanajongea meza yenye mshumaa na kuwasha. Wakati wa tendo hilo watu wanashangilia na wimbo ufaao mfupi waweza kimbwa.


Baada ya kuwasha Mshumaa wa Ndoa, wote kwa pamoja wanapimagoti mbele ya huo mshumaa wa Ndoa na kusali sala ifuatayo wakiwa wamepiga magoti.

Ee MUNGU Mwenyezi wa milele, / ndiwe uliyeiweka ndoa, / kusudi wanadamu waongezeke, / na watu wa ndoa wasaidiane na kutulizana. Tunakushukuru kwa kutuunganisha / katika Sakramenti ya Ndoa / kwa kifungo kisichofunguka,/ tupate kuwa wawili katika umoja. Kwa hiyo / twakuomba kwa matumaini, / utujalie neema / za kutunza daima mapendano na saburi, / amani na mapatano; / ututie nguvu ya kuzuia yote / yanayovunja uaminifu na usafi wa ndoa yetu.

Utuimarishe / tuweze kuwalea vema / watoto utakaotujalia, / kuwafundisha uchaji wa MUNGU / na usafi wa mwenendo,/ na kuwakinga na makwazo na mabaya yote.

Utusaidie kuvumilia kwa saburi / masumbufu ya maisha. Ubariki kazi na shughuli zetu halali; / uongoze mioyo yetu, / tupate kutumia vema vitu vya dunia, / tusije tukapoteza mema ya mbinguni.

Utujalie kusaidiana kwa uaminifu / katika mema yote, / na hivyo twende pamoja / njia iendayo mbinguni; / na baada ya kuaga dunia, / tuungane nawe mara moja,/ milele mbinguni. Tunaomba hayo / kwa njia ya KRISTO BWANA wetu. / Amina.

Baada ya sala hiyo, yanafuata maombi.


Maombi

P. Ndugu wapenzi, tuiombee familia hii mpya ya (F) na (F), kusudi neema na upendo ambayo MUNGU amependa kukamilisha na kutakatifuza ndani yao vikue siku kwa siku. Tuwaombee tukiitikia:

Kiitikio: Bwana wabariki wanaharusi hawa.

i. Ndugu zetu hawa bwana harusi na bi Harusi, waliounganika sasa kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, wajaliwe daima nguvu na afya. Ee BWANA.

ii. MUNGU abariki agano lao kama alivyopenda kuibariki harusi ya Kana ya Galilaya. Ee BWANA.

iii. Upendo wao kamili wenye baraka awaletee amani na msaada; waweze kutoa ushuhuda wa kweli wa ukristo wao. Ee BWANA.

iv. Kwa ajili ya majirani na marafiki zao na wote wale waliowasaidia Bwana harusi na BI Harusi katika kufanikisha ndoa yao, ee MUNGU uwajalie baraka na neema zako, ili waendelee kuiombea ndoa hii iwe na heri na baraka. EeBWANA.

v. Watu wa ndoa wote waliopo hapa, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waamshe ndani yao neema ya Sakramenti ya Ndoa na waziheshimu kiaminifu ndoa zao. Ee BWANA.

vi. Kwa ajili ya marehemu wa wanaharusi hawa, ee MUNGU uwajalie uzima wa milele mbinguni. Ee BWANA.

P. Ee Bwana, upende kuwajaza bwana harusi na bi harusi roho wako wa upendo ili wawe roho moja na moyo moja wala wasitenganishwe tena na jambo lolote lile. Hao ambao umewaunganisha na kuwajaza baraka yako wasipate madhara yoyote. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

Misa inaendelea kama kawaida.

Baada ya maombi misa inaendelea kama kawaida kwa kutoa mchango misa. Wakati wa kutia sahihi shahada za ndoa, wanaharusi watatia sahihi zao kwenye meza iliyoandaliwa na si Altareni.

Inafaa wanaharusi wachukue mshumaa wa ndoa na wawe wanauwasha na kusali mbele yake kila mwezi tarehe ya ndoa yao.





Friday, March 19, 2010

Hii ni Kwaresima

Nini maana ya Kwaresima?
Kwa Kilatini na Kiitaliano neno Kwaresima lilimaanisha “40” yaani siku 40 za kufunga za wiki kati ya Jumatano ya Majivu hadi Jumamosi Kuu. Kwa Kijerumani Kwaresima maana yake “Kipindi cha kufunga.”

Kwaresima ilianzaje?

Kabla ya kuona Kwaresima jinsi ilivyoanza, ni vizuri kuongea kidogo kuhusu Sikukuu ya Pasaka ili tuweze kupata mwanga wa kuelewa mwanzo wa kipindi hiki muhimu cha Kwaresima.

Habari Njema yatuambia kwamba YESU KRISTO alifufuka “Siku ya kwanza ya juma.” “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.” (Mt.28:1) Hii ni kwasababu Wakristo walianza kukutana pamoja kwa sikukuu ya ufufuko wa BWANA kila wiki sio Jumamosi kama Wayahudi, bali siku iliyo fuata. “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza -`maneno yake hata usiku wa manane.” (Mdo.20:7). “Siku ya Kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake: ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja.” (1Kor.16:2), siku ambayo Warumi waliita “Siku ya Jua”. Mara moja jina hilo lilibadilika na kuwa “Siku ya BWANA”

Kanisa la mwanzoni halikusherehekea sikukuu kama vile Noel, Sikukuu kwa heshima ya Mama Bikira Maria au sikukuu yeyote ile. Kulikuwepo na adhimisho la ufufuko wa BWANA kila wiki na hakuna zaidi.

Miaka mingi ikapita kanisa likiwa katika hali hii. Baadaye kulikuwepo na hitaji la kusherehekea tukio la kiini cha imani yetu kwa namna ya pekee. Wakristo waliona umuhimu wa kuwa na muda kwa sikukuu ya kwanza kati ya sikukuu zao yaani “Jumapili ya Pasaka”, ambayo ilifikiriwa kama “Mama wa Jumapili zote”, “Mama wa skikukuu zote”. Waliiona sikukuu hiyo kama “Malkia wa sikukuu zote, wa Jumapili zote, na kiujumla kama Malkia wa siku zote za mwaka. Tangu mwanzoni mwa karne ya pili, Jumuiya zote za Kikristo walikuwa wanasherehekea sikukuu hii ya Pasaka. Sherehe zilikuwa zinahitimishwa na kusanyiko la sala lililofanyika usiku na kumalizikia na Ekaristi. Ushiriki wa kwenye ibada hiyo, ulichukuliwa kama ni kitu muhimu sana kwa mkristo.



Kuanza kwa Kwaresima

Wote tunafahamu kwamba, ufanisi au mafanikio yoyote ya sikukuu au ya jambo lolote yanategemea sana maandalizi yake. Miaka miambili hivi baada ya KRISTO, Wakristo walitaka kuvuna matunda ya kiroho ya Paska kwa wingi. Ili kufanikisha hili, walianzisha utamaduni wa kuwa na siku tatu kabla ya Pasaka kwa sala, tafakari na kufunga kwa nia ya kuonyesha masikitiko yao juu ya kifo cha YESU KRISTO. Kutokana na ukubwa na umuhimu wa sikukuu hii, mbali ya kuona umuhimu wa maandalizi, walitafuta njia za kuongeza muda wa furaha na utajiri wa kiroho utokanao na Pasaka. Hivyo walianzisha “Wiki Saba,” yaani siku 50 za Pentekoste ambapo walisherehekea na kuzipitisha siku hizo kwa hali ya furaha. Askofu Mt. Ireneus alisema kuwa muda huo wa siku 50 ni kama Sikukuu ya Siku moja yenye umuhimu sawa na Jumapili. Katika kipindi cha siku za Pentekoste, sala zilikuwa zinasaliwa hali wamesimama, kufunga kulikatazwa na sakramenti ya ubatizo ilikuwa ikiadhimishwa. Ni kama vile sikukuu ya Pasaka ilidumu kwa kipindi chote cha siku 50. Miaka 150 ilipita na mwishoni mwa mwaka 350 B.K., Wakristo waliona kama siku tatu hazikutosha kwa maandalizi ya sikukuu kama hii. Hivyo waliongeza hadi kufikia siku 40. Hivi ndivyo Kwaresima ilivyoanza.

Kwa nini siku 40?

Tunaposema kuku wanne au kilo saba za mchele tuna maana kama ilivyo yaani kuku wanne na kilo saba za mchele. Si zaidi au pungufu.

Namba au tarakimu mbalimbali tunazokutana nazo katika Biblia zinaashiria lugha za picha na siyo kuchukulia katika thamani ya kuhesabu. Hivyio basi, tunapokutana na namba kama 40 huenda isimaanishe 40 kama tunavyo hesabu fedha. Kati ya maana nyingi zilizotolewa kwa namba 40, kuna moja yenye maana ya pekee, inamaana ya kipindi cha maandalizi cha kutosha kisichokuwa na muda maalum, kwa tukio kubwa. Kwa mfano , Gharika ilidumu kwa siku 40 usiku na mchana…na ilikuwa ni maandalizi ya ubinadamu mpya; Waisraeli walitumia muda wa miaka 40 jangwani…maandalizi ya kuingia nchi ya ahadi; watu wa Ninawi walifunga na kufanya kitubio siku 40…maandalizi ya kupokea msamaha wa MUNGU; Elia alitembea kwa siku 40 mchana na usiku…kama maandalizi ya kufika mlima wa MUNGU; Musa na YESU walifunga kwa siku 40 mchana na usiku… kama maandalizi kabla ya kuanza utume wao. “Kisha ROHO alimwongoza YESU mpaka jangwani ili ajaribiwe na ibilisi. Akafunga siku arobaini usiku na mchana, na mwishoe akaona njaa” (Mt.4: 1-4)

Natumaini hadi hapo tumeelewa nini maana ya namba 40. Je, ni siku ngapi ambazo zinahitajika kwa ajili ya maandalizi ya sikukuu kubwa kuliko zote za kikristo? Bila shaka ni 40. (Kuanzia Jumatano ya majivu hadi Jumamosi Kuu ukiondoa Jumapili zote) Siku 40 ni muda wa kutosha wa kufanikisha kitu fulani chema, kizuri na chenye thamani.

Lengo la Kwaresima ni nini?

Lengo kuu la Kwaresima ni kufanya upya maisha yetu ya kiroho na kutufanya kuwa watu ambao MUNGU anataka tuwe yaani ni kipindi chenye kutupatia utakatifu, tukikumbuka kuwa sote tumeitwa kuwa watakatifu kama BABA yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu (Mt. 5:48). Ni kipindi cha kuuvua utu wetu wa kale na kuvaa utu mpya. Kwani tunasoma:- “Mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unao haribika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho na nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa na MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli. Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake…Mwibaji asiibe tena…Neno lolote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema na kufaa…tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi.” (Efe.4:22-32.)

Kwaresima kwa hakika ni kipindi pia cha kuachana na matendo ya mwili. “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo;” (Gal.5:19 – 20)

Kwa ufupi Kwaresima ni kipindi cha kuachana na maisha ya dhambi na kurudi kwa MUNGU kwa kuishi maisha yanayompendeza MUNGU kwa njia ya kufanya toba ya kweli isiyo ya mazoea, na malipizi yasiyo ya nje tu, bali hasa mapinduzi ya kiroho. Katika kipindi hiki tunalazima ya kubadili hali yetu ya ndani. Badala ya kujitafuta wenyewe na kufuata mapenzi yetu, inatupasa sisi kumwelekea MUNGU na kuyatimiza mapenzi yake katika mawazo, maneno na matendo yetu.

Nguzo tatu kuu za Kwaresima ni:

i. Sala. “Wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani. Usali mbele ya BABA yako aliye sirini; na BABA yako aonaye sirini atakujazi.” (Mt. 6:6)
Kupata muda wa sala pamoja na MUNGU. Sio tu kunena maneno ya sala fulani, lakini pia kumsikiliza MUNGU akizungumza mioyoni mwetu. Kumuomba MUNGU nguvu ya kubadilika, yaani uongofu wa kweli. Ndiyo maana tunaambiwa. “Tubuni na kuiamini Injili”. Hayo ndiyo MUNGU aombayo kwetu wakati wa Kwaresima. MUNGU anatuita kutoka kwa dhambi, na tuupokee ujumbe wake kwetu – Injili, na kuwa waamninfu kuishi kadiri ya Injili. Ni wakati pia wa kuhudhuria misa mara kwa mara kwa ibada na uchaji, kuhudhuria ibada mbalimbali, kama vile Baraka ya Sakramenti Kuu, Kuabudu Ekaristi Takatifu, kusoma Neno la MUNGU na kuliishi baada ya kuyatafakari maneno hayo ya MUNGU ambayo ndiyo sauti yake MUNGU na kutumia muda wetu kwa mambo ya ki-MUNGU yaliyo matakatifu.

ii. Kufunga. “Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso wako ili usionekane na watu ukifunga, ila na BABA yako aliye sirini; na BABA yako aonaye sirini atakutuza.” (Mt. 6:17-18). Kufunga sio tu kujinyima kutokunywa pombe, kutokula chakula, kutovuta sigara n.k. Kifupi ni kwamba kufunga kuondokana na ubinafsi wetu na kuwafikiria na kuwasaidia wenye shida. Uovu hauwezi kushindwa bila kujitoa nafsi na bila kutoa na kuwapa wahitaji vile tuvipendavyo. MUNGU hapendezwi na kufunga tu, bali upendo kwa wanaoteseka utusukume na kufunga tupendavyo kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji. Hivyo kuna mahusiano makubwa sana kati ya kufunga na ukarimu. Kufunga lazima kuendane na ukarimu. Kufunga bila ukarimu huo ni mfungo tasa.

iii. Kutoa Sadaka. “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu kusudi mtazamwe nao. Bali wewe utoapo sadaka hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wa kuume; na BABA yako aonaye kwa siri atakujazi.” (Mt. 6:1) Hayo yanamaanisha kwamba usidai shukurani wala malipo kwa wema wowote uwatendeao jirani zako kwa sadaka yako. Malipo utakayopata uyatazamie tu kutoka kwa BABA yako wa mbinguni. Kutoa tunachojinyima kwa kumsaidia KRISTO anayeteseka kwa wenzetu. Kushirikiana na wengine tulivyo navyo kama vile fedha, nguo, chakula, ama kuwakaribisha wahitaji nyumbani.

Hivyo basi, Mazoezi tunayofanya katika kipindi cha Kwaresima kama kusali zaidi, kusikiliza au kusoma Neno la MUNGU, kutenda matendo ya huruma kwa wahitaji, kufunga chakula na kujihinisha kinywaji pamoja na kuzuia tamaa potovu za mwili wetu, yawe na kusudi la kuibadili hali yetu, kutufanya kuwa na upendo zaidi na huruma kwa wenzetu na kutufanya tuweze kuunganika zaidi na KRISTO MFUFUKA. Tumvue mtu wa zamani katika nafsi zetu na tumvae mtu mpya, yaani KRISTO Mfufuka.

Nini makusudi ya kufunga?
YESU alifunga ili awape wanadamu mfano au kielelezo halisi na sahihi cha kuiga, na apate kuokoa roho zetu. Watu wawe na namna bora ya kufanya malipizi, kuuadibisha na kuutumikisha mwili na tamaa kwa kuwa anatenda dhambi.

Nani anapaswa kufunga?
Inatubidi tujiangalie sana kwani miili yetu ni midhaifu na myepesi kwa kutenda dhambi na kuipeleka roho motoni. Tusiiendekeze miili yetu, bali tuitawale kwa kufuata maadili ya kimungu na kuinyima madai yake, ambayo ni kishawishi kinachotupeleka upotevuni. Tunapoamua kufuata njia hii, hakika, KRISTO atatuimarisha na kutuongoza kwenye uzima wa milele; na kutupa neema ya kupambanua mema na dhambi, huku tukielekea uzimani. Mdomo unao nena dhambi, na mwili unaotenda dhambi, sherti vyote vitende pia mema, siyo dhambi.

Mtu asiyetenda dhambi hana haja ya kufunga. Lakini hakuna mtu anyefikia utu uzima ambaye hatendi dhambi machoni pa MUNGU hata Wacha MUNGU wana dosari. Kwa hiyo, kila mtu afunge kufidia dhambi zake. Tusipofunga kuna hatari kubwa ya kuungua moto. Ni vizuri waamini wote wafunge ili kulipia fidia ya dhambi zinazotendwa. Tumwabudu KRISTO kwa unyofu na unyenyekevu, ili kwa huruma yake kuu atusamehe dhambi zetu na adhabu tunazostahili.

Ngazi tatu za kufunga chakula:

(a) Ngazi ya kwanza, ni kuacha chakula kimoja fulani, au kitu kingine unachopendelea. Kufunga huku ni rahisi hata kwa watoto. Kwa mfano, kuacha kula nyama au kunywa soda yoyote kwa kipindi kizima cha Kwaresima; au kula chakula bila chumvi, au kunywa chai bila sukari kwa kipindi kizima cha mfungo. Huu ni mfungo rahisi.

(b) Ngazi ya pili, ni kuacha kabisa kula siku nzima. Hii ni ngazi ya kawaida, yaani mfungo wa kawaida. Huku ni kula mlo mmoja tu kwa siku hadi utosheke. Yawezekana ikawa ukala mlo wa mchana au wa jioni tu. Asubuhi au jioni (au asubuhi na mchana) ule kidogo sana. Katikati ya hapo usile chochote tena wala kunywa chochote.

(c) Ngazi hii ya tatu ni ya wale wanaotaka kufanya malipizi makali zaidi. Huu ni Mfungo mkali. Katika ngazi hii ya kufunga watu wengi huaacha kabisa kula na kunywa siku nzima, wakawa na huo mlo mmoja tu. Wanaotaka malipizi makali zaidi siku ya kufunga chakula, asubuhi pokea Ekaristi Takatifu, na wala usiguse chakula au kinywaji chochote kingine. Mchana unaweza kula slesi moja (kipande) tu ya mkate na unywe glasi moja tu ya maji ya kawaida. Jioni pia ule slesi moja ya mkate na unywe glasi moja tu ya maji. Na endapo utaamua kutokula kabisa na kutokunywa kabisa hadi asubuhi kesho yake, itampendeza zaidi Mwenyezi MUNGU. Hii ndiyo toba ya kweli.

Tukumbuke kwamba kile tunachofunga kiwasaidie wasiojiweza. Si kufunga kwa nia ya kuweka akiba ili baada ya mfungo uweze kutumia wewe mwenyewe! La hasha. Huo si mfungo wenye kuleta faida kiroho, bali ni mfungo tasa.

Kuacha kula nyama Ijumaa Kuu na Ijumaa nyingine za mwaka.

Ufungapo au uachapo kula nyama, funga kweli na acha kweli kula nyama kwa dhati kwa toba ya dhambi. Vinginevyo utakuwa unajidanganya mwenyewe. Papo uutolee mfungo wako na kutokula nyama huku kwa Mwenyezi MUNGU, kwamba unafanya hivyo kwa kudhamiria. La sivyo utadhania unafunga na unaacha kula nyama kwa manufaa ya kiroho wakati unashinda tu na njaa ! Kuacha kula nyama maana yake ni kula vyakula vitokanavyo na ardhi tu; ndivyo vyakula vya mfungo. Acha kula kila aina ya nyama, na mafuta yanayotokana na wanyama. Usile nyama, mayai, mafuta ya wanyama, siagi na jibini, wala maziwa. Kula vitu vyovyote vitokanavyo na wanyama au ndege hurahishisha mfungo wako. Kumbuka pia kwamba siku za kufunga na kuacha kula nyama, uwe macho sana, maana shetani mshawishi atakuja kupima utashi wako. Shinda mwili (njaa na kiu) wako, mshinde shetani anyekuongoza dhambini. Jambo la muhimu hasa ni kwamba matendo hayo yote yatendeke kwa ajili ya BWANA. Tuyafanye kama alama ya kwamba tunataka kurudi kwake. Yawe ni matendo kati ya MUNGU na mimi. Kwa sababu hiyo lazima kulinda siri ya jambo lolote tutakalo tenda. “BABA yako aonaye sirini atakujazi.”

Nini thamani na maana ya kujinyima jambo fulani ambalo kimsingi ni zuri na inafaa kwa ajili ya afya ya mwili?

Thamani na maana ya kufunga tunaiona na kupata mfano kwa YESU. Ni vema tukumbuke kwamba Kwaresima inatukumbusha siku 40 za mfungo wa BWANA wetu jangwani, alivyofanya kabla ya kuanza Utume wake hadharani, (Mt. 4:1-2). Pia, kama Musa alivyofunga kwa siku 40 usiku na mchana kabla ya kupokea zile Mbao za Sheria (Kut. 34:28). Eliya naye alifunga kabla ya kukutana na BWANA katika Mlima Horeb (1 Wafal. 19:8), YESU vile vile kwa njia ya sala na kufunga, akijitayarisha kwa ajili ya majukumu yaliyokuwa mbele yake, alituonesha tangu mwanzo mapambano makali dhidi ya Shetani.

Hivyo basi, Maandiko Matakatifu na mafundisho yote ya desturi za ukristo yanafundisha kuwa mfungo ni msaada mkubwa katika kukwepa dhambi na vishawishi vinavyoweza kutupeleka katika dhambi yenyewe. Kwa kuwa kila mmoja wetu anaelemewa na dhambi na mafuatano yake, kufunga kumependekezwa kwetu kama njia ya kurudisha urafiki wetu na MUNGU. Hivi ndivyo alivyofanya Ezra (8:21), walivyofanya watu wa Ninawi (Yona 3:9).

Je, unajua mfungo wa kweli ni upi?
Mfungo wa kweli kama YESU alivyorudia mahali pengi, ni kufanya mapenzi ya Baba aliye Mbinguni, “na BABA yako aonaye sirini, na atakujazi” (Mt. 6:18). Mfungo wa kweli unaelekezwa katika kula chakula cha kweli; yaani “kufanya mapenzi ya MUNGU” (Yn. 4:34).

Hivyo basi, kama katika Kwaresima hii UMEAMUA kweli kusali, basi funga; kama unafunga, onesha huruma; kama unataka maombi yako yasikiwe, sikiliza maombi ya wengine. Endapo hufungi masikio yako kwa wengine, unafungua masikio ya MUNGU kwa ajili yako.

Kwa hakika mfungo unaleta faida za kimwili, lakini kwa Mkristo mfungo upo kwa ajili ya “Tiba” ya kuponya yale yote yanayouzuia mwili kutekeleza utashi wa MUNGU. Pia kufunga ni njia ya kuonesha “huzuni” (1 Sam 31:13; 1 Fal 21:27; Neh1:4); toba (1 Sam 7:6; Yoe 2:12; Dan 9:3-4) au hali ya “unyofu katika maombi” (2 Nya 20:3-4; Ezra 8:23).

Mpenzi msomaji wa kijitabu hiki, nakutakia Kwaresima njema na mfungo wenye heri na toba ya kweli mbele za MUNGU kwa kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha yetu ili kufungua mifereji ya neema na baraka katika mtu binafsi, familia na Jumuiya. Tukumbuke kwamba dhambi huzuia baraka na neema toka kwa MUNGU hata kurudisha nyuma maisha yetu ya kiroho na maendeleo katika familia. Hivyo, katika kipindi hiki cha Kwaresima tukitumie kwa kufanya toba ya kweli kimatendo ili kuondoa vikwazo vyote vinavyo zuia maendeleo yetu kiroho na ya kifamilia kwa kuwa tayari kumegwa kuwa chakula kwa wengine kwa njia ya ukarimu wetu. Tujitahidi katika kushiriki Ibada ya Njia ya Msalaba ikichukuliwa katika mtazamo wa kufanya toba na kuomba msamaha kwa MUNGU. Kushiriki Sakramenti vema hasa Sakramenti ya upatanisho ili mfungo, na toba yetu vipate kibali machoni pake MUNGU na kushiriki matakatifu.
MUNGU akubariki na kukulinda. Nakutakia kwaresima njema.

“Wakati umetimia na ufalme wa MUNGU umekaribia, Tubuni na kuiamini Injili.” (Mk 1:16).



NJIA YA MSALABA

Njia ya Msalaba ni ibada ya Mateso na Kifo cha KRISTO. Tunasafiri naye kiroho kutoka kwenye nyumba ya Pilato hadi Kalvari. Tunakumbuka yote yaliyotukia tangu alipohukumiwa hadi alipozikwa karibuni. Tunafanya ibada hii kwa kuwa karibu na YESU anayeteseka kwa ajili yetu na kuwa karibu na Bikira MARIA Mama wa Mateso. Hivyo, tufikiri juu ya ubaya wa dhambi zetu na kuzijuta na kudhamiria kuziacha kweli. Pili, tufikiri juu ya Fumbo la Mapendo ya YESU kwa BABA yake na kwetu sisi wanadamu. Ibada hii itusaidie kuonja wokovu uliotujia kwa Mateso, Kifo na Ufufuko wa Mkombozi wetu, YESU KRISTO.




Sala mbele ya Altare
Ee, Mkombozi wangu, ninakuja leo kufuata njia ile uliyoshika siku ya kufa sadaka yetu. Nimetubu dhambi zangu zote; ninataka kugeuza mwendo wangu; ninaomba kwako niwapatie roho za waamini marehemu waliomo toharani, rehema zote zilizotolewa na Kanisa kwa Njia ya Msalaba. Nawe MARIA Bikira Mtakatifu, uliyefuata njia ile nyuma ya mwanao YESU, uniangalie kwa wema, unitie Moyo Mkuu, nisipende dhambi tena, nikivumilia kazi na usumbufu na mateso na matukano yatakayonipata.

**************
Umekosa nini we YESU,/ Kushtakiwa bure kwa Pilato
Wenye kustahili hukumu, Si wewe, si wewe BWANA, ni sisi.

KITUO CHA KWANZA - YESU anahukumiwa afe
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Pilato anamhukumu YESU ingawa haoni kosa lake, anawaogopa Wayahudi. Anabembeleza urafiki wa Kaysari. Ee YESU usiye na kosa, hata mimi ningeweza kutenda mema mengi, lakini naogopa macho ya wenzangu, na maneno yao. Ee BWANA, uniima-rishie utashi wangu, nijitegemee katika kushika madaraka yangu.

BABA yetu… – Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**************
Ole Msalaba huo mzito, / Apagazwa mwana mpenzi wa MUNGU. / Mwili waenea mateso, / Alipa, alipa madhambi yetu

KITUO CHA PILI - YESU anapokea msalaba
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

YESU anakubali kuelemewa na msalaba kwa ajili ya wokovu wa watu. Ndivyo anavyonifundisha moyo wa sadaka, moyo wa kujitolea na kujisahau kwa ajili ya wengine. Ee YESU wangu mkarimu, mimi pia ninao msalaba wangu: jirani zangu, mwenzangu wa ndoa, watoto, wazazi wangu, kazi zangu, joto, baridi, njaa, kiu, vishawishi, magonjwa na matatizo mengine ya maisha, wajibu wangu kwa MUNGU, kwa umma na kwa Kanisa. Hayo yote ni msalaba. Unipe ukarimu wako ee YESU, niyapokee bila kunung’unika, na kuyabeba vema.

BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**************
Ona Muumba mbingu na nchi, / Yupo chini mzigo wamwelemea, / Na mtu kiumbe chake kwa ukali, / Ampiga, ampiga bila huruma.

KITUO CHA TATU - YESU anaanguka mara ya kwanza
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

YESU amedhoofika sana, anaanguka chini, kisha anasimama, anaendelea na safari ya ukombozi. Ee YESU uliyeanguka chini ya msalaba kwa ajili ya udhaifu, ukasimama tena; usiniache katika tamaa nikianguka dhambini, bali nisimame mara moja, nikufuate.

BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**************
Huko njiani we MARIA, / Waonaje hali ya mwanao, / Ni damu tupu na vidonda, / Machozi, machozi yamfumba macho.

KITUO CHA NNE - YESU anakutana na mama yake
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Wote wawili mama na mwanawe wanaumia sana moyoni kwa ajili ya dhambi zangu. Ee YESU, Mwana wa MARIA, unitilie moyoni mwangu upendo na ibada kwa Bikira MARIA; unijalie na ulinzi wake, nisitende dhambi tena.

BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**************
Kwa Simoni heri ya kweli, / Mimi pia YESU nisaidie, / Kuchukua mzigo wa ukombozi, / Kuteswa, kuteswa pamoja nawe.

KITUO CHA TANO - Simoni wa Kirene anamsaidia YESU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Nausifu ukarimu wa Simoni wa Kirene. Ee BWANA unijalie ukarimu kama huo, niitikie nami wito wa kukusaidia kuchukua msalaba. Nitoe zaka na michango yote ya uenezaji wa dini; nijitolee mimi mwenyewe katika kazi ya maendeleo ya dini. Uwajalie vijana wengi wito wa Upadre, waweze kuchukua msalaba pamoja nawe kwa ajili ya wokovu wa dunia. Uwaimarishe viongozi wa dini. Ustawishe moyoni mwa waamini wote mwamko wa utume.

BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**************
Uso wa YESU Malaika, / Betlehemu walikuabudu, / Bahati yake Veronika, / Kupangusa, kupangusa Mfalme wa Mbingu.

KITUO CHA SITA - Veronika anapangusa uso wa YESU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Mama huyu ni kinyume kabisa cha Pilato. Veronika anajua analopaswa kutenda, na analitenda bila kujali macho na maneno ya makundi ya watu waovu. Ee YESU, uliyemtuza Veronika zawadi ya picha ya uso wako juu ya kitambaa, unijalie ushupavu na ujasiri wake wa kutenda mema, ili roho yangu ipambwe kwa chapa ya uungwana na utakatifu wako.

BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

Wakimvuta huku na huku, / Wauaji wanamchokesha bure, / Chini wanamtupa bado kwa nguvu, / Aibu, aibu yao milele.

KITUO CHA VII - YESU ANAANGUKA MARA YA PILI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU uliyelegea mno kwa mateso makali, unapoanguka mara ya pili kwa ajili ya udhaifu wa mwili, wanionya kwamba hata mimi naweza kurudi dhambini kwa udhaifu wa moyo. Nipe basi neema ya kuepuka nafasi za dhambi na visa vyenye kunikwaza na kunirudisha dhambini.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amni. Amina.

Wanawake wa Israeli, / Msilie kwa sababu hiyo, / Muwalilie hao kwa dhambi, / Upanga, upanga ni juu yao.

KITUO CHA VIII - AKINA MAMA WANAMLILIA YESU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Asanteni sana akina mama kwa moyo wenu wa huruma. Ee YESU uliyetulizwa na wanawake, unipe moyo wa kuwaheshimu akina mama wote. Uwaite na wasichana wengi waingie utawa, ili watulize moyo wako Mtakatifu kwa sala na sadaka zao.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

Mwokozi sasa ni ya tatu, / Waanguka chini ya msalaba, / Katika dhambi za uregevu, / Nijue, nijue kutubu hima.

KITUO CHA IX - YESU ANAANGUKA MARA YA TATU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU unayezidi kudhoofika kwa mateso unaanguka mara ya tatu, upate kunistahilia neema ya kuutiisha mwili wangu na kuusulibisha, licha ya kuepuka nafasi za dhambi. Mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno starehe, anasa na tafrija. Ee YESU mwema, nisaidie kuufuata mfano wa Mtakatifu Paulo, niutese mwili wangu na kuutumikisha, ili nipate siku moja tuzo mbinguni.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

Muje Malaika wa Mbingu, / Funikeni mwiliwe kwa huruma, / Vidonda vyake na utupu, / Askari, askari wamemvua.

KITUO CHA X - YESU ANAVULIWA NGUO
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Askari wanamvua kwa nguvu nguo yake, iliyogandamana na madonda yake; wanayaamsha mara moja mateso yote aliyoteswa tangu mwanzo. Ee YESU, unayavumilia mateso makali haya, upate kunifundisha kuuvua kwa nguvu moyoni mwangu urafiki mbaya, au kitu kingine chochote kile kinachoharibu urafiki wa MUNGU, hata ikipasa kutoa sadaka kubwa.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

Hapo MKRISTO ushike moyo, / BWANA wako alazwa msalabani, / Mara miguu na mikono, / Yafungwa, yafungwa kwa misumari


KITUO CHA XI - YESU ANASULIBIWA MSALABANI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU uliyepigiliwa misumari msalabani, nakutolea akili na utashi wangu, vifungwe pamoja na miguu yako, nipate kuwaza, kusema na kutenda siku zote yale tu yanayolingana na utukufu wa msalaba wako Mtakatifu. Ee YESU, mimi ni mfungwa wako. Nisaidie kuimarisha kifungo hicho kwa sala, Sakramenti na fadhila za KiKRISTO.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**********
YESU mpenzi nakuabudu, / Msalabani unapohangaika, / Nchi yatetemeka kwa hofu, / Na jua, na jua linafifia.

KITUO CHA XII - YESU ANAKUFA MSALABANI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU uliyekufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu, unijalie niichukie dhambi, nisiishi kamwe katika dhambi. Nifahamu kwamba nilipobatizwa kwa jina lako, nilibatizwa katika mauti yako ili utu wangu wa kale usulibishwe nawe, mwili wa dhambi uangamizwe nisitumikie tena dhambi.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**********
Mama MARIA mtakatifu, / Upokee maiti ya Mwanao, / Tumemwua kwa dhambi zetu, / Twatubu kwake na kwako.


KITUO CHA XIII - YESU ANASHUSHWA MSALABANI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU uliyeshushwa msalabani baada ya kufa, unijalie nidumu katika maisha ya kujitoa sadaka mpaka siku ya kufa kwangu. Nielewe na kukubali kwamba baada tu ya kufa ndio mwisho wa vita na mashindano ya KiKRISTO.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

Pamoja nawe kaburini, / Zika dhambi na ubaya wa moyo, / YESU tuwe Wakristo kweli, / Twakupa twakupa sasa mapendo
.
KITUO CHA XIV - YESU ANAZIKWA KABURINI
- Ee YESU, tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.

Ee YESU, ulizikwa kaburini, ukafufuka siku ya tatu. Mimi pia nilizikwa pamoja nawe kwa njia ya ubatizo katika mauti yako. Kwa vile wewe ulifufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa BABA, unijalie nami nifufuke, yaani nishike mwenendo mpya, mwenendo wa uzima wa milele.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

**********
Katika roho yangu BWANA, / Chora mateso niliyokutesa, / Nisiyasahau madeni, / Na kazi, na kazi ya kuokoka.

(Hiari yako - Mbele ya Altare)

KITUO CHA XV - YESU AMEFUFUKA
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu

Habari njema aliyotuletea YESU ni kwamba baada ya kila Ijumaa Kuu huja sikukuu ya Pasaka; kwamba punje ya ngano isipoanguka ikafa, hukaa hali hiyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa maozo mengi. Twakushukuru, ee YESU, kwa mateso yako, lakini twakushukuru hasa kwa ufufuko wako, kwa kuwa huo ndio unaotupa hakika ya kuwa hatukuzaliwa kwa ajili ya mateso na maumivu, bali kwa ajili ya heri ya milele.

BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.

*********
SALA YA MWISHO
Mbele ya Altare: YESU wangu, kwa uchungu wote ulioona juu ya msalaba, na kwa kuzimia kwako kwa ukali wa mateso, unijalie nguvu ya kuvumilia kwa moyo taabu zote sasa na saa ya kuzimia kwangu. Nawe MARIA Mamangu, kwa uchungu wote ambao moyo wako umejaa ulipomwona mwanao mpenzi kuinama kichwa na kuzimia, unifadhili nife kifo chema.

SALA YA KUMWOMBA YESU ALIYETESWA
YESU wangu,/ kwa masikitiko uliyoyaona hata ya kuzimia roho,/ na kwa jasho la damu ulilotoka kwa sababu ya dhambi zangu,/ unitie uchungu wa kweli juu ya makosa yangu! YESU wangu, / kwa msongo wa moyo uliouona kutolewa na Yuda,/ unifanyizie nikae amini kwako,/ nisikutoe bado vile nilivyofanya mpaka leo!/ YESU wangu, uliyefungwa kama mtu mwovu,/ niunganishe nawe kwa vifungo vya mapendo yako! YESU wangu,/ kwa madharau uliyodharauliwa, / na machukizo uliyochukizwa mbele ya Ana,/ Kaifa na Herodi,/ uniwezeshe kuvumilia kwa saburi matukano nitakayotukanwa na watu! / YESU wangu, kwa maumivu uliyovumilia mwilini mwako ulipopigwa fimbo nyingi mno,/ nijalie nguvu ya kustahimili maumivu ya ugonjwa, / na kukataa furaha zote mbaya!/ YESU wangu, /kwa mateso uliyoona ulipotiwa taji la miiba,/ unipe neema ya kutokubali tena mawazo yoyote ya majivuno na ya uchafu!/ YESU wangu, /uliyechukua msalaba wako mzito kwa ajili ya dhambi zangu, / unitie moyo mkuu, / nikubali kwa uvumilivu taabu na sulubu zote za maisha yangu! / YESU wangu, uliyemwaga damu yako yote juu ya msalaba kwa ajili yetu,/ nifanyizie niwe hai kwa ajili yako tu!/ YESU wangu, kwa kiu kikali ulichoona kwa ajili yangu,/ nifanyizie nisikukasirishe tena kwa kupenda mno chakula au kileo!/ YESU wangu, kwa uchungu wote uliouona juu ya msalaba,/ na kwa kuzimia kwako kwa ukali wa mateso,/ nijalie nguvu za kuvumilia kwa moyo taabu zote saa ya kuzimia kwangu!/ Nawe MARIA Mama yangu, kwa uchungu wote ambao moyo wako umejaa / ulipomwona Mwanao mpenzi akiinama kichwa na kuzimia,/ unifadhili nife kifo chema! Amina.

Nafasi ya Waamini Walei Katika Mwaka wa Mapadre

NAFASI YA WAAMINI WALEI KATIKA MWAKA WA MAPADRI
Na. Pd. Rochus Conrad Mkoba

Utangulizi
Mwaka wa Mapadri ni mwaka kwa Kanisa zima ambapo waamini wanaalikwa kuwaenzi na kuwasindikiza Mapadri katika maisha na utume wao kwa njia ya sala, mashauri mema, na sadaka zao, kwaajili ya utakatifu wa Mapadri, ongezeko la miito ya Kipadri pamoja na kuendelea kuthamini dhamana ya Mapadri katika maisha ya Familiya ya MUNGU ili watimize wajibu wao na hatimaye tuwe na mapadri wanaojitoa katika wito wao.

Waamini wapendwa, ni vema mtambue fika kwamba mmezaliwa mara ya pili kwa maji na ROHO MTAKATIFU (rej. Yn 3:8; Mt28:19). Mnalishwa chakula cha Mbinguni, Neno la MUNGU, Sakramenti, na mnalelewa hadi kuingia mbinguni kwa huduma takatifu za mapadri. Hivyo, mnapowaombea Mapadri wenu katika mwaka huu wa Mapadri ili wawe watakatifu, wakati huo huo mnajiombea ninyi wenyewe pia kuwa watakatifu hapa duniani na hadi mbinguni. Kwa hakika ndugu wapendwa waamini walei, wito wenu ni kuombea Mapadri, Kanisa na familia zenu, ili tupate miito mitakatifu.

Lengo na dhumuni la Mwaka wa Mapadri
Lengo na dhumuni la mwaka wa Mapadri, uliotangazwa na mpendwa wetu Papa Benedikti XVI kuadhimisha miaka 150 ya kifo kitakatifu cha Cure’ wa Ars, Mt. Yohane MARIA Vianney (1786-1859), ni kuombea utakatifu wa Mapadri wakimtazama Mt. Yohane MARIA Vianney msimamizi wa Maparoko aliye mfano wa kuigwa katika maisha ya kipadre hasa kwa kukazia toba na wongofu wa ndani na umuhimu wa fumbo la Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kipadre.

Waamini wote Wakatoliki, wenye mapenzi mema, ambao huwapenda mapadri wao na wangependa kuwashuhudia wakiwa wanafurahi, waadilifu na wachangamfu katika kazi zao za kitume kila siku, wanaalikwa na Mama Kanisa kushiriki kwa dhati katika Mwaka huu kuwaombea mapadri wao kwa kusali, sadaka, kufanya tafakari, kusherehekea, na kutoa heshima kwa mapadri wao na kwa hiyo uwe mwaka unaotoa fursa kuendeleza ushirikiano na urafiki baina ya mapadri na jamii zilizoaminishwa chini ya uchungaji wao.

Kwa nini Waamini wanaalikwa na Baba Mtakatifu kuwaombea Mapadri?
o Ili, wawe waaminifu kwa ahadi zao za kipadre walizotoa wakati wanawekwa wakfu na kurudia kila mwaka wakati wa Alhamisi Kuu, kwenye misa ya Krisma ya Wokovu. Waamini wanaalikwa kuwaombea sana Mapadri kwani Baba Mtakatifu amesikitika na kusema kwamba Mateso makuu ya Kanisa yanatokana na dhambi zinazotendwa na wachungaji wasio waaminifu kwa kondoo wa KRISTO; kwa njia ya mafundisho yao potofu au kwa kuendelea kuishi katika dhambi ya mauti. Hivyo Baba Mtakatifu anawaalika Mapadri kutubu na kuongoka kwa kukimbilia huruma na upendo unaobubujika kutoka Moyo Mtakatifu wa YESU na daima wakiomba ulinzi wake, ili kutowadhuru wale ambao Mama Kanisa amewapatia ili waweze kuwaongoza na kuwakomboa.

o Ili, wawe waaminifu, watakatifu na wahudumu wa upendo na huruma ya KRISTO inayoleta mvuto kwa waamini, kwa njia ya ushuhuda hai wa maisha yao.

o Ili, waweze kuwaka moto wa upendo wa shughuli za kichungaji, wakijitahidi kumuiga YESU KRISTO, kuhani Mkuu, kwa ajili ya majitoleo ya kweli.

o Ili kudumisha upendo na Ibada kwa Bikira MARIA, uliokuwa na mvuto wa pekee katika maisha ya Mt. Yohane MARIA Vianney, kiasi kwamba, mnamo mwaka 1836, akawa mtangulizi kuhusu Mafundisho Sadikifu ya Bikira MARIA Mkingiwa Dhambi ya Asili. Hivyo Mapadri wanatakiwa kuwajengea waamini wao Ibada kwa Bikira MARIA atakayewasindikiza Makleri katika Mwaka wa Mapadri, ili kweli waweze kuwa ni mfano wa kuigwa.

o Ili, kuwamegea waamini Mkate wa uzima na kielelezo cha upendo, kuwaondolea watu wake dhambi zao pamoja na kuwaongoza kwa niaba ya YESU mwenyewe na katika utume wao waweze kujitambulisha na KRISTO.

o Ili, waweze kuyatolea maisha yao kama sadaka safi na inayopendeza machoni pa MUNGU.

o Ili, kuheshimu na kuthamini neema ya wito, maisha yao ya wakfu na utume wao.

o Ili, waweze kutekeleza vizuri wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa MUNGU.

o Ili waamini na watu wenye mapenzi mema kufahamu maana ya wito wa Kipadre na dhamana yake ndani ya Kanisa Katoliki.

o Ili, Mapadri waweze kujijengea fadhila za kuwa wachungaji wema, wasikivu na wenye muungano wa dhati na KRISTO kuhani Mkuu, kwa njia ya Sala, Sakramenti, Tafakari ya Neno la MUNGU ili hata katika ubinadamu wao, waweze kumpeleka MUNGU, kilele cha utajiri wote kwa watu duniani.

o Ili kutambua wajibu wao kwamba, wao ni KRISTO wa pili katika utume wao.

o Ili, MUNGU aliye mwasisi na kiongozi wa Kanisa, awategemeze Mapadri kwa neema yake siku zote, ili watimize wajibu wa Kipadri kwa moyo mwaminif.

o Ili, MUNGU azidi kuwafanya mapadri wawe watumishi, na mashahidi wa upendo na ukweli wa kimungu hapa duniani, na wahudumu waaminifu wa upatanisho.

o Ili, MUNGU awafanye Mapadri wawe wachungaji halisi, wanaowapatia waamini mkate wenye uzima na neno la uzima, ili wakue katika umoja wa mwili wa KRISTO.


Kauli Mbiu ya Mwaka wa Mapadri.
“Uaminifu wa KRISTO, Uaminifu wa Mapadri”

Kauli mbiu ya mwaka wa Mapadri ni; “Uaminifu wa KRISTO, uaminifu wa Mapadri”, changamoto kwa Mapadri kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwa waaminifu katika wito na utume waliokabidhiwa na Mama Kanisa katika maisha yao.

YESU aliamua kuwatumia Mapadri hata katika mapungufu yao ya kibinadamu kuendeleza utume wake wa ukombozi ulimwenguni, kwa hakika anasema kardinali Justin Rigali, Askofu Mkuu wa Jimbo la Philadelphia, “hii ni zawadi na fumbo linalopita ufahamu wa akili ya mwanadamu.”

Mwaka wa Mapadri ni mwaka unaopania kuleta mabadiliko ya ndani kwa Mapadri wote, ili waweze kutolea ushuhuda wa maisha yao unaohitajika katika ulimwengu wa leo, ambapo Baba Mtakatifu anawaalika Mapadri wenzake kufanya hija ya maisha yao ya Kiroho hatua kwa hatua, kwa kukazia umuhimu wa zawadi ya maisha na wito wa Kipadre kwa ajili ya Kanisa na jamii kwa ujumla.




Kwa nini katika Mwaka wa Mapadri Baba Mtakatifu anawahimiza Mapadri kuiga mfano wa Mt. Yohane MARIA Vianney?

Mapadri wanaalikwa na Baba Mtakatifu kuiga mfano wa Mt. Yohane MARIA Vianney kwa moyo wake uliosheheni huduma kwa MUNGU na jirani. Alikuwa mtu mnyenyekevu na daima alitambua wito wake wa Kipadre na dhamana ya maisha yake kwa ajili ya watu aliokuwa amekabidhiwa na Mama Kanisa kuwamegea watu wa MUNGU huruma na Upendo wa MUNGU. Ni mtu aliyewajibika bila kikomo, akawa tayari kuyamimina maisha yake kwa ajili ya upendo. Alitambua kwamba, ametumwa kuumwilisha uwepo wa KRISTO na ushuhuda wa kazi inayokomboa, kimsingi wito wa maisha ya Mt. Yohane MARIA Vianney ufanisi wake kwenye shughuli za kichungaji ulijichimbia zaidi katika utakatifu wa maisha pamoja na kukutana na waamini, waliohitaji msaada wake wa kipadre.

Alijiwekea utaratibu wa kutembelea wagonjwa, familia, kutoa mahubiri, kusherehekea sikukuu mbalimbali kuwahudumia watoto yatima. Alionesha umakini kwa ajili ya kuwapatia watoto Katekesi pamoja na kuanzisha vyama vya Kitume kwa kuwashirikisha walei katika shughuli zake za kichungaji.

Ushuhuda wa Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu, Adhimisho la Ibada ya Misa na maungamo, yote haya yaliweka chachu ya maisha yake kwani daima alijisemea moyoni mwake kwamba, maisha ya Kipadre yanapata msingi katika Ibada ya Misa Takatifu, inayopaswa kupewa kipaumbele, kwani ni kielelezo cha juu kabisa cha maisha na utume wa Kipadre.

Mt. Yohane MARIA Vianney alionesha upendeleo wa pekee katika adhimisho la Sakramenti ya Upatanisho, na alijitahidi kukaa kwenye kiti cha maungamo kwa muda wa masaa 16 kwa siku! Aliwafariji waliovunjika moyo, akawaimarisha walegevu na kuleta mabadiliko na wongofu wa ndani kwa kuwaonesha upendo na huruma ya MUNGU, akawa ni hospitali ya maisha ya Kiroho, ili kuwasaidia waamini kuondokana na dhambi katika maisha yao.

Alifanikiwa kuyatajirisha maisha yake kwa njia ya mikesha, na kufunga; alikuwa anatoa kitubio kidogo kwa waamini waliokuwa wanaungama kwake, sehemu nyingine ya kitubio aliifanya yeye mwenyewe akashiriki mateso ya wadhambi katika Parokia yake.

Mt. Yohane MARIA Vianney aliridhika kutoa yote kwa ajili ya upendo kwa jirani bila ya kutaka kuwa na kishawishi cha kujilimbikizia mali kwa ajili ya mafao yake mwenyewe. Useja, ulimwezesha kuyainua macho yake kwa KRISTO katika Tabernakulo na kwamba, Utii, ulikuwa ni kielelezo cha huduma ya hali ya juu kabisa kwa MUNGU.

Hivyo kwa kuiga mfano wa Mt. Yohane MARIA Vianney Mapadri wataweza kuuishi kikamilifu wito wao wa Kipadre kwa kuzingatia mashauri ya Kiinjili na kutoa mwanga wa Jumuiya za Kikristo kuchanua kama maua ya kondeni.

Kwa kukazia hilo, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika mwaka huu wa Mapadri amewaweka Mapadri wote chini ya ulinzi wa Bikira MARIA na kuwakumbusha kwamba, YESU KRISTO anawategemea na kwamba wanapaswa kuwa ni wajumbe wa Matumaini, Upatanisho na Amani.

REHEMA kutolewa kwa Waamini Watakaotekeleza Masharti wakati wa Mwaka wa Kipadre, 16 Juni, 2009 hadi 19 Juni, 2010.

Tamko lilitolewa na Kardinali James Francis Stafford, Mwenyekiti wa Toba ya kitume amesema kwamba, Kanisa linatoa rehema kamili kwa waamini katika mwaka wa Mapadri.

Kabla ya kujua masharti ambayo mwamini ataweza kujipatia rehema kamili, ni vizuri kufahamu maana ya rehema.

Nini maana ya rehema?
Rehema ni msamaha mbele ya MUNGU wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwisha futwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiandaa vyema anaweza kuupata kwa kutekeleza masharti yaliyowekwa na tendo fulani la Kanisa ambalo kimsingi ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya KRISTO na ya watakatifu.

Rehema Kamili.
Hivyo, Rehema kamili inatolewa kwa waamini waliotubu na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, wakisali kwa ajili ya kuwaombea Mapadri kwa YESU KRISTO na Zaburi kwa ajili ya moyo Mtakatifu wa YESU, hao watapata rehema kamili baada ya kuondolewa dhambi zao na kusali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu: kwa siku za ufunguzi na ufungaji wa mwaka wa kipadre, siku ya kumbukumbu ya miaka 150 tangu afariki dunia Mt. Yohane MARIA Vianney; Alhamisi ya kwanza ya mwezi au siku nyingine iliyoidhinishwa na Askofu mahalia kwa ajili ya maeneo yanayotumika na wakristo.

Kwa wagonjwa, wazee na wale wote kutokana na sababu msingi watashindwa kutoka nyumbani kwao, kwa moyo wa toba ulio mbali kabisa na dhambi, wakiwa na nia ya kutaka kutekeleza masharti mengine yaliyotajwa hapo juu mapema iwezekanavyo watapata rehema kamili, ikiwa kama watasali kwa ajili ya kuombea utakatifu wa maisha ya Kipadre, na kutolea mateso na mahangaiko yao kwa MUNGU kwa njia ya maombezi ya Bikira MARIA Malkia wa Mitume.

Rehema ya muda.
Rehema ya muda, itatolewa pia kwa waamini watakapokuwa wanasali kwa Ibada sala ya BABA Yetu, Salam MARIA na Atukuzwe BABA mara tano, au sala nyingine zilizoidhinishwa kwa ajili ya heshima kwa Moyo Mtakatifu wa YESU. (Tazama sala hizo hapo chini) Tamko hili linafanya kazi tu kwa kipindi cha mwaka wa Kipadre.

Hitimisho
Waamini mnaalikwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kushiriki kikamilifu katika kuwaombea na kuwaenzi Mapadri wenu kwa njia ya sala, Mashauri mema, tafakari, na sadaka ili muweze kuwaona Mapadri wenu mnaowapenda wakiwa na furaha katika huduma na utume wao; watakatifu na watu wenye uso wa tabasamu, kwa sababu wanajitoa kwa ajili ya MUNGU na jirani zao. Pia, mbali ya kuwaombea, mnaalikwa na Mama Kanisa kuwasaidia mapadri wenu kujikimu kwa kuwapatia mahitaji muhimu kwani wakati mwingine mapadri wanaishi katika hali ya umasikini mkubwa uliokithiri na kukabiliwa na madhila katika sehemu nyingi mbalimbali za dunia. Jipatie rehema kwa kuwaombea na kuwasaidia mapadri wako hususan katika mwaka huu wa Mapadri.

MUNGU awabariki kwa upendo mkubwa katika jukumu hili; Mama BIKIRA MARIA, Malkia wa Makleri, awaombee kila mmoja wenu, ninyi wapenzi Waamini Wakatoliki.

******************

Sala mbalimbali za kuwaombea Mapadri, watawa, miito na za Moyo Mtakatifu wa YESU

Kwa ajili ya Mapadri
Uwalinde, nakuomba BWANA mpendwa, uwatunze kwani ni wako – Mapadri wako ambao maisha yao yanawaka mbele ya madhabahu yako takatifu. Uwalinde kwani wako ulimwenguni, japo wao si wa ulimwengu huu, wakati wote raha za dunia zinapowashawishi, zinapowavuta – watunze katika moyo wako. Watunze, wafariji katika nyakati za upweke na maumivu, wakati maisha yao yote ya sadaka kwa ajili ya roho yanapoonekana kuwa si kitu. Watunze, na kumbuka Ee BWANA, hawana mwingine isipokuwa wewe, lakini bado wao wana mioyo ya kibinadamu tu, wakiwa na mapungufu ya kibinadamu. Waweke bila doa kama vile hostia, ambayo kila siku wanaigusa – kila wazo lao na neno na matendo, BWANA mpendwa wabariki.

Kwa ajili ya kuwaombea Mapadri
Kanisa linatushauri kuwaombea Mapadri na watumishi wa Kanisa hasa Alhamisi au Jumamosi ya kwanza ya mwezi.

K. Ee YESU utupendae, uliwaambia mitume wako: “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi.” Basi, uchague vijana wema wanaosikia sauti yako ukiwaita wawe Mapadri wako na watumishi wa Kanisa lako.

Kiitikio: Ee BWANA, ulijalie Kanisa lako Mapadri waaminifu (Baada ya kila ombi).

K. Uwasaidie wanafunzi wote wa upadre. Uwape neema yako ili wakufuate siku zote, washinde taabu na vishawishi vyote katika njia ya kufikia kikomo chao cha upadre.

K. Uwafundishe wazazi wakristo wakae vema na kitakatifu, kusudi wapate watoto wema wapendao kutolea nguvu zao kwa ajili yako katika kazi ya upadre.

K. Uwajalie Mapadri wetu neema za kipadre ili waweze kutimiza sawasawa kazi zao kwa wokovu wa nchi yetu na kwa sifa ya Kanisa lako takatifu.

K. Ee YESU, Mkombozi wa makabila yote, usikie maombi yetu; Ufalme wako uenee katika nchi zote. Unayeishi na kutawala daima na milele. W. Amina.

Sala ya kila siku kwa kupata Mapadri na Watawa wema.
Kiongozi: YESU mchunga mwema, umefika kuwatafuta na kuwaokoa wote waliopotea. Umeuweka upadre katika Kanisa ili uendeshe ukombozi wako nyakati zote. Twakuomba sana uwapeleke watu wa kazi shambani mwako. Uwaamshe Mapadri wema katika Kanisa lako. Utuletee watawa wanaume na wanawake wenye bidii. Wote walioteuliwa nawe waitikie mwito wako, lakini wasioitwa wasijiingize patakatifu pako.

Wote: Uwaimarishe Mapadri na watawa wote/ wapate kuutimiza mwito wao. / Ubariki taabu na kazi zao. / Uwafanye wawe kama chumvi, / dunia isipate kuoza; / wawe kama mwanga, / wenzao wapate kuangazwa kwa mfano na maonyo yao. / Uwape elimu, saburi, uthabiti / waongeze sifa yako, / waeneze ufalme wako mioyoni mwa watu / waongoze waamini wao kwa uzima wa milele. Amina. MARIA, Malkia wa mitume, utuombee.

Kwa nia hiyo inafaa sana kuabudu Ekaristi Takatifu muda wa saa nzima siku ya Moyo Mtakatifu wa YESU.

Kuwaombea Mapadri
Ee BWANA, upeleke Mapadri wema na watakatifu katika Kanisa lako. Ee MARIA, Malkia wa Mapadri, utuombee, utujalie na Mapadri wengi watakatifu.

Sala ya kuiombea Miito
Ee YESU mpole, ulivumilia mateso makali mpaka kufa kwa ajili ya kutuokoa sisi binadamu, tunakuomba utujalie tupate Mapadri, Mabruda na Masista wengi walio watakatifu. Tunawahitaji sana katika Parokia yetu, Jimbo letu, Nchini mwetu na katika Kanisa lote. Uwajalie vijana wetu, wavulana na wasichana, neema ya kuitikia wito wako mtakatifu. Uwape hamu ya kueneza neno lako. Uwajalie pia neema ya kuwa wasikivu wakati wa malezi yao katika Seminari, katika nyumba za kitawa, na mahali popote watakapoishi. Hatimae waufikie wito wao. Amina. BABA yetu, Salamu MARIA, Atukuzwe BABA.

Sala ya kuiombea Miito ya Upadre
Ee YESU KRISTO, ukumbuke kulijalia taifa lako viongozi katika njia ngumu za dunia hii ili wawe kitulizo cha wachaji wa MUNGU. Uwafanye wawe mifano, uwaangaze watambue neema yao, uimarishe utashi wao wasishindwe na vishawishi. Usiwaache kutoroka msalaba, na uwajalie wazazi wao kutambua ubora wa kukutolea watoto wao. Uwape wenye mali moyo wa kuwasaidia kwa fedha wanafunzi wa upadre, uwajalie walimu wao wachochee wito. Uwape elimu, saburi, uthabiti na tabia njema, wakaongeze sifa yako, wakaeneze ufalme wako, wakaongoze watu wako kwako. Ee MUNGU, uyape mataifa yote Mapadri wanaotafuta zaidi mapenzi yako kuliko ya wanadamu, furaha zao kuliko za kijamii, kusudi wawe baba wa Parokia wanaowakumbuka zaidi maskini na fukara, wakosefu, wagonjwa na wasio na raha mioyoni. Ee Bikira MARIA, Malkia wa Mitume, uwe mwombezi wetu kwa Mwanao. Mama wa Kanisa, utusikilize na kutuombea. Amina. (Papa Pius XII).

Sala ya kuwaombea wanafunzi wa utawa.
Ee MUNGU, ulimwengu wote ni wako. Tangu zamani za kale ulichagua watu kwa utumishi wako wa pekee. Hata sasa huwa unamvuta mmoja mmoja kwa sauti yako nyanana ili akutumikie wewe peke yako. Unamwita kwako ili ajinyime heri ya mapendo ya ndoa kwa nadhiri ya useja na usafi wa moyo, apate kuambatana nawe kwa namna ya pekee; ajinyime mali na nyumba yake mwenyewe kwa nadhiri ya ufukara na hivyo kwa moyo wake wote akutamani wewe na kukuelekea; ajinyime hiari ya kufuata utashi wake kwa nadhiri ya utii, akijinyima tena na tena katika hamu yake kubwa ya kujitawala. Umetaka mtawa akuelekee wewe akikufuata kwa namna ya pekee ili wewe peke yako uwe utajiri wake na rafiki yake. Ee BWANA, ninastaajabia ukuu wa wito wako. Ninakuomba, ITA! Uwahimize wale unaowaita wakusikilize na kukufuata; na wale uliokwisha waita uwaimarishe katika maisha yao. Uwajalie watu wanaofuata wito wako heri ile unayowafumbulia wale wanaojitoa kabisa kwako. Amina.

Kuwaombea Mapadri
Ee MUNGU Mwenyezi wa milele, Kwa mastahili ya Mwanao YESU KRISTO
Na kwa ajili ya upendo wako kwake,

a. Uwahurumie Mapadri wa Kanisa takatifu, licha ya cheo chao kikubwa,
Mapadri wanafanana na viumbe wengine, na ni watu dhaifu.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.

b. Tunakusihi kwa huruma yako isiyopimika, uwape moto wa upendo mtakatifu,
na uwashe mioyo yao kwa upendo huo.

c. Ikupendeze, Mwenyezi MUNGU, kuwasaidia; usiwaache waanguke wala kutetereka katika wito wao.

d. Ee BWANA YESU, tunakusihi: uwaimarishe Mapadri wa Kanisa lako
wanaokutumikia kwa uaminifu, wanaolinda kundi la malisho yako,
na kutukuza utukufu wako.

e. Uwahurumie Mapadri wanaoteswa, walio kifungoni, walio katika upweke,
na wanaolemewa na mateso.

f. Uwahurumie Mapadri walio vuguvugu na wanaoyumba katika imani yao.
Wote ni mali yako; ikupendeze kuwaangazia hao pia, uwape nguvu na uwafariji.

g. Uwainue Mapadri wagonjwa na wanaokufa; na wale wanaoteswa toharani uwape rehema yako mapema.

h. Ee BWANA YESU, ninakukabidhi Mapadri wa ulimwngu mzima. Ikupendeze kuwatunza kwa namna ya pekee Padre aliyenibatiza na wote walioniondolea dhambi; waliotolea sadaka takatifu ya misa kwa ajili yangu na kuigeuza hostia takatifu ili kulisha roho yangu.

i. Ninakukabidhi pia, BWANA YESU, Mapadri wote walioyaondoa mashaka yangu,
walionitunza katika unyonge wangu, walioongoza jitihada zangu na kunifariji
katika mateso yangu.

Tuombe: Kwa mastahili ya mema hayo na mema yote ambayo watumishi wako wanayatenda katika huu utumishi wao mtakatifu, ninawaombea Mapadri wote msaada na huruma yako, MUNGU unayeishi na kutawala daima na milele. Amina.

Sala kwa Moyo Mtakatifu wa YESU
Kadiri watu wanavyozidi kuukana na kuukufuru UMUNGU wako, ndivyo tutakavyozidi kukuabudu kwa heshima zaidi, Ewe Moyo wa MUNGU uliyejifanya Mtu.

Kadiri watu wanavyozidi kuyakataa na kuyapinga mafundisho yako, ndivyo tutakavyozidi kuwa imara katika kuyasadiki na kuyatangaza. Ee Moyo wa MUNGU na Mwalimu wetu.

Kadiri watu wanavyodharau mamlaka ya Kanisa lako, ndivyo tutakavyoyatii. Ee Moyo wa MUNGU na Kiongozi wetu.

Kadiri watu wanavyozama katika mambo ya kidunia ndivyo tutakavyozidi kukoleza akili zetu na roho katika Injili yako: Ee Moyo wa MUNGU wetu Msulubiwa.

Kadiri watu wanavyozidi kudharau na kuzikufuru Sakramenti Takatifu, ndivyo tutakavyozidi kuziheshimu na kuzipenda. Ee Moyo MUNGU na Rafiki yetu!

Kadiri Ibilisi anavyozidi kunyang’anya roho za watu, ndivyo tutakavyozidi kujitahidi kueneza Ufalme wako. Ee Moyo wa MUNGU na Mfalme wetu!

Kadiri Unavyozidi kuchukiwa ndivyo tutakavyozidi kukupenda. Ee Moyo wa MUNGU wetu Mpendwa na Mpendelevu Utusaidie. AMINA.

Sala ya majitoleo kwa Moyo Mtakatifu wa YESU
Ee Mpenzi Moyo Mtakatifu wa YESU, ninakupenda sana na ninakupa moyo wangu. Nisaidie kumpenda MUNGU. Nisaidie kumpenda jirani yangu kama mtoto wa MUNGU. Nisaidie kujipenda mwenyewe kama mtoto wa MUNGU. Ninajitolea kwako, ninaomba neema ya kukupenda na kukutumikia kama unavyostahili. AMINA.

Sala ya Moyo Mtakatifu wa YESU (majitoleo binafsi)
Ee Moyo Mtakatifu wa YESU, ninajitolea kwa Moyo wako Mtakatifu. Twaa nafsi yangu yote nigawe niwe vile vile Ulivyo. Ifanye mikono yangu iwe yako, miguu yangu iwe yako, Moyo wako uwe wangu. Niwezeshe kuona kwa macho yako, kusikia kwa masikio yako, kuongea kwa midomo yako, kupenda kwa Moyo wako, kuelewa kwa akili yako, kutumia kwa mapenzi yako na kujitolea kwa nafsi yangu yote.

Nifanye niwe nafsi yako ingine. Ee Moyo Mtakatifu wa YESU, nijalie ROHO MTAKATIFU Anifundishe kukupenda na kuishi kwa msaada wako, pamoja nawe ndani yako na kwa ajili yako.

Njoo ewe ROHO MTAKATIFU fanya mwili wangu uwe hekalu lako. Njoo ukae nami daima. Nipe Mapendo makubwa sana kwa Moyo Mtakatifu wa YESU ili nimtumikie kwa Moyo wangu wote na roho yangu yote na kwa nguvu zangu zote. Twaa uwezo wangu wote, mwili na roho. Tawala tamaa zangu zote mawazo ya ndani na mahangaiko ya moyo. Twaa akili yangu hekima na utashi kumbukumbu na mawazo. Ee roho wa Mapendo nipe neema nyingi za kunifaa, nipe utimilifu wa fadhila zote. Ongeza imani yangu, imarisha matumaini yangu, zidisha tegemeo langu na amsha mapendo yangu. Nijalie utimilifu wa mapaji yote saba, matunda na heri nyingi. Ewe Utatu Mtakatifu ifanye roho yangu iwe mahali pako patakatifu. AMINA.

Sala ya Moyo Mtakatifu wa YESU kuomba msaada
Ee Moyo Mtakatifu wa YESU uliyepata uchungu mkubwa mno, ulipopata mateso siku ile katika bustani ya Getsemani. Ulichoka kwa jinsi mwili wako ulivyoanguka kifudifudi. Ooh! Namna Moyo wako ulivyostuka hata uso wako ukatoka jasho la damu. Utuhurumie ee Moyo ujuaye sikitiko, Moyo uliochomwa kwa mkuki, Moyo ulioshibishwa matusi na michomo yote ya dunia. Moyo ujuaye huzuni na mahangaiko, Moyo uliopata kila aina ya aibu, Moyo uliofanywa mahututi. Loo! Jinsi ulivyoumia, ulivyougua pole sana Ee YESU wangu na kwa kuumizwa kwako sisi sote tumepona.

Ee YESU Maradhi yangu ni yako. Ee YESU twende pamoja katika bustani ya Getsemani. Baba maumivu yangu ni yako yanauma. Ee YESU wangu ikiwezekana nisiwe kama ulivyosema, “Baba ikiwezekana kikombe hiki nisikinywe, lakini siyo kama nitakavyo mimi bali mapenzi yako yatimizwe”. AMINA.

Ibada kwa ajili ya kuwatakatifuza mapadri kwenye familia au Jumuiya

Waamini wakisha kusanyika, au wanafamilia wakishakusanyika, kiongozi wa ibada anafungua ibada kwa maneno yafuatayo:

Kiongozi: Kwa jina la BABA na la MWANA na la ROHO MTAKATIFU

Wote: Amina

Kiongozi: Utukuzwe ee BWANA, uliyetukusanya pamoja kusali kwa ajili ya kuwatakatifuza mapadri wetu.

Wote: Amina! Mapendo yako kwa ajili yetu ni ya milele.

Kiongozi: Katika Mwaka huu wa Mapadri, Baba Mtakatifu anatuomba tutumie muda wa kutosha wa kusali kwa ajili ya kuwatakatifuza Mapadri. YESU, Kuhani Mkuu, Mchungaji wa milele na Kiongozi wa roho zetu, leo kuliko wakati wowote ule mwingine, anawataka mapadri wawe watakatifu, mapadri wanaolingana na moyo wake. Mapadri ni wahudumu wa KRISTO. Wakiunganika na Maaskofu wao, mapadri wanaadhimisha mafumbo ya imani, hasa Sadaka ya BWANA. Utendaji wao ni muhimu na wa msingi kwa maisha ya Kanisa, na unawataka wajitoe kabisa wawe na moyo usiogawanyika, ili taifa la MUNGU liweze kuwatambua kama wafuasi wa KRISTO ambaye alikuwa kila kitu kwa watu wote. Ndugu, tumwombe MUNGU Mwenyezi awaimarishe katika wajibu wao wa ukarimu wale aliowaita katika upadri

Kiitikio: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, BWANA”



Kiongozi: Sifa kwako YESU! Kwa kuutoa mwili wako Msalabani ulikamilisha sadaka za kale, ukawa kwa ajili yetu Altare, Sadaka na Kuhani. Hivyo ulituwezesha kuondokana na utumwa wa dhambi na kuingia katika ule utukufu unaotutangaza kuwa taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa ufalme wako, ili tuweze kuutangazia ulimwengu kwamba wewe ndiwe BWANA.

Kiitikio: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, BWANA”

Kiongozi: Sifa kwako, ee YESU! Chemchemi ya ukweli na uzima. Kulisikiliza neno lako na kupokea Mkate mmoja wa Ekaristi kunajenga kanisa. Katika Fumbo hili kuu unawalisha na kuwatakatifuza watu wako, ili imani moja na upendo mmoja uangaze na kuwaunganisha wanadamu waliotawanyika popote ulimwenguni.

Kiitikio: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, BWANA”

Kiongozi: Sifa kwako, ee YESU! Mchungaji Mwema, uliyeutoa uzima wako kwa ajili ya kondoo wako. Ulijenga Kanisa juu ya mitume liwe kwa karne zote ishara inayoonekana ya utakatifu wako, na kwa jina lako kuwaletea watu wote kweli zinazoongoza kwenye uzima wa milele.

Kiitikio: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, BWANA”

Kingozi: Sifa kwako, KRISTO! Kuhani wa milele, Mtumishi mtii, Chemchemi itoayo uzima wa mafumbo yote. Uwajalie karama na vipaji mbalimbali wale uliowachagua kuwa wachungaji wa Mafumbo yako matakatifu, na unaye walisha ili katika kila sehemu ya ulimwengu sadaka timilifu iweze kutolewa, na waweze kujenga kwa Neno na Sakramenti jumuiya ya Agano Jipya, hekalu la utukufu wako.

Kiitikio: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, BWANA”

Neono la MUNGU
Masomo yafutayo yanaweza kutumika kwa tafakari: YESU na BABA (Yn 17:1-5); YESU na Wanafunzi wake (Yn 17:6-17); YESU na Kanisa (YN 17:20-26)

Baada ya somo na tafakari, yanafuata maombi


Maombi
Kiongozi: Ndugu, tusali kwa imani kwa njia ya YESU KRISTO, Kuhani Mkuu wa milele, Mchungaji wa roho zetu, ili awahifadhi katika imani, matumaini na mapendo wale wote aliowaita katika huduma ya upadre.

Kiitikio: Uwatakatifuze watu wako, ee BWANA.

YESU, ambaye moyo wako ulichomwa kwa mkuki ulitoa damu na maji na ukamzaa mchumba wako kanisa, utuoshe na kututakatifuza. Ee BWANA

YESU ulisema; “Na uhai wa milele ndio huu: ni kukujua wewe uliye peke yako, MUNGU wa kweli na kumjua yule aliyemtuma” (Yn 17:3). Ulitunze ndani ya mapadri wako hitaji la kukujua wewe na kukujulisha kwa wengine. Ee BWANA.

YESU, Neno la MUNGU uliyesema; “Anayewasikia ninyi, ananisikia mimi”. Utusaidie kutambua sauti yako katika sauti za mapadri wako. Ee BWANA.

YESU, Mfalme na kiini cha mioyo yote, umewaaminisha wahudumu wako kazi ya upatanisho; utuoneshe kina cha huruma yako na uwaokoe wanaume na wanawake na nyakati zetu kwa agano la upendo. Ee BWANA.

YESU ulisema; “Mavuno ni mengi, lakini wafanyakazi ni wachache. Mwombeni BWANA wa mavuno awapeleke watenda kazi shambani mwake” (Mt 9:37-38). Ulijalie Kanisa lako miito mipya na mitakatifu ya upadri na utawa. Ee BWANA.

Hapa inawezekana kuongeza maombi mengine
BABA yetu…
Tuombe: Ee YESU mpole, ulivumilia mateso makali mpaka kufa kwa ajili ya kutuokoa sisi binadamu, tunakuomba utujalie tupate Mapadri, Mabruda na Masista wengi walio watakatifu. Tunawahitaji sana katika Parokia yetu, Jimbo letu, Nchini mwetu na katika Kanisa lote. Uwajalie vijana wetu, wavulana na wasichana, neema ya kuitikia wito wako mtakatifu. Uwape hamu ya kueneza neno lako. Uwajalie pia neema ya kuwa wasikivu wakati wa malezi yao katika Seminari, katika nyumba za kitawa, na mahali popote watakapoishi. Hatimae waufikie wito wao. Amina.
Kiongozi: Tunaukimbilia……
Kiongozi: Atukuzwe BABA…
Kiongozi: Kwa jina la BABA…… (Wote) Amina

Wednesday, July 29, 2009

Kupokea EKARISTI TAKATIFU mkononi kusihimizwe

EKARISTI TAKATIFU
Uwepo wa YESU wa Ekaristi huanza dakika ya mageuzo na hudumu muda wote ambao maumbo ya Ekaristi yapo. KRISTO ni wote kabisa katika kila umbo, na ni wote kabisa katika kila sehemu yao, kwa jinsi hii kwamba kumega mkate hakumgawanyi KRISTO. (Paulo VI) Hata kichembe kidogo namna gani KRISTO ni wote kabisa. “Basi akawaambia, “Amin, Amin,nawaambieni: Msipokulamwili wake mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; name nitamfufu siku ya mwisho.” (Yoh. 6:53-54)

Kuna mambo ambayo yanashughulikiwa tu na Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee=Kutupa au kuchukua au kuwanayo Ekaristi Takatifu kwa nia ovu.

KUPOKEA EKARISTI TAKATIFU MKONONI NI KUSIHIMIZWE.
Cha msingi ni kwamba: Wakatoliki wanaokomunika waungame kwanza dhambi zao ndipo wamaribie YESU wa Ekaristi (Mfalme wa wafalme, BWANA wa mabwana, MUNGU mwenye enzi kuu amabye huwezi kumfananisha na yeyote awaye yule) na wampokee wakiwa wamepiga magoti mdomoni. (Zamani) Wasikufuru kwa kumpokea YESU wa Ekaristi wakiwa katika hali ya dhambi. Kupokea kwa kustahili na kupata mafaa ya Komunyo, kunahitaji maandalizi ya dhati kwa upande wa mkonunikaji:
i. anapaswa kutokuwa na dhambi ya mauti yoyote,
ii. anapaswa kuwa na huzuni kwa dhambi ndogo zote na kujitahidi kuzishinda
iii. anapaswa kufunga chakula au vimiminika (isipokuwa maji) angalau saa moja kabla ya kupokea,
iv. anapaswa kushiriki kikamilifu katika Ekaristi ambamo anapokea.


· Papa Paul II, Nov. 1980, Ujerumani. “Kuna barua ya kitumeinayoruhusu kupokea Ekaristi Takatifu kwenye mkono. Lakini nawaambieni sipendekei zoezi hilo wala si shauri.”

· Mama Teresa wa Calcuta, India, alipohojiwa mwaka 1989 akiwa New York kuhusu kile anachofikiri kuwa ni jambo baya zaidi katika dunia ya sasa, yeye alijibu bila kusita na kusema; Popote ninapokwenda dunia nzima, kitu abacho kinanifanya niwe na huzuni sana ni kuwaona watu wakipokea Ekaristi Takatifu kwa mikono.” Katika shirika lake masita wake wote walikuwa wakipokea Ekaristi Takatifu mdopmoni.

· Askofu Juan Rudolf aliwahi kusema; “Kwa kupokea Ekaristi Takatifu mkononi, muujiza unatakiwa wakati wa kugawa Ekaristi ili kuepuka vipande vya hostia visianguke au kubaki mkononi mwa mpokeaji. “

Kuthibitisha hili ni barua ya toba kwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo VI aliyoiandika Charles Andre akiungama kwa kutupa au kusababisha kutupwa kwa takribani Komunyo 60,000 tangu mwaka 1980 ahdi 1991 na kusababisha hostia hizi kuendelea kukaknyagwa. Kwa vile alifanya vile bila kujali. Hata wapokeaji nao hawakujali.

Katika uchunguzi wake, aligundua kuwa wastani wa vipande 3.68 vya komunyo hubakia kwa mpokeaji. Hii ni kwa vile alifanya jaribio kwa kutumia hostia zilizotoka kwenye viwanda vinavyotengeneza hostia kwa kiwango cha hali ya juu sana, (Ubaora).

Alifanya uchunguzi akiwa na mtoto wake. Walinunua hostia zilizokuwa na ubora wa hali ya juu ambazo kingo zake zilikuwa imara. Waliosha mikono yao vizuri sana na kuikausha vema. Kisha, alimpokelesha mtoto wake mkonopni naye akachukua kwa vidole akala. Kisha walihesabu vipande vilivyokuwa kwenye vidole vya mkomunishaji, vya juu ya kiganja, na vidole vya aliye komunika. Katika hostia 25 walipata matokeo haya = vipande 92 vilionekana kwa macho. 27 + 47 + 18 = 92.

Hebu tufikirie tunatupa hostia ngapi? Mara nagapi tunazikanyaga pale mbele tunpokwenda kupokea? Kufuru ya aina gani hiyo? Je, tuendelee hivyo? Je, sisi tunaotupa, tunaokanyaga bila kujali tunatarajia kukumbatiwa na kupongezwa mbinguni na YESU kwa kufuru hiyo?

Mfalme wa Japani katika karnekadhaa zilizopita alipokuwa akiwaua wakatoliki wa kweli kwa ukatili aliwalazima kukana imani yao kwa kukanyaga msalaba wa mbao bila mwili. Japo alikuwa mtu mwovu kiasi hicho, hakuthubutu kuwaambia wakanyage Ekaristi Takatifu. Je, sisi?


Matokeo ya kugawa Ekaristi Takatifu mkononi
· Mtu mmoja alikuwa nazo nyumbani kwake 200 na alizipini ukutani akichora umbo la kipepeo.

· Wengine waliichukua na kuipasua ili waone kama damu itatoka kisha wakatupa chooni.

· Mwingine aliichukua na kuisahau mfukoni hadi ilipooneka Dry cleaner kwenye mfuko wake wa suruali.

· Mwingine walimkuta nazo 17 akiziuza kwa Franck moja kwa kila Ekaristi.

· Miaka kadhaa iliyopita Ekaristi zaidi ya 200 zilikamatwa uwanja wa ndege wa Dar zikisafirishwa nje.

· Mwezi Februari mwaka wa 2007 nilipokea barua ikinionya kuwa watu wanachukua Ekaristi na kwendanazo. Nilithibitisha hili baada ya mwamini mmoja kuniambia kwamba mtu mmoja alichukua Ekaristi na kwenda nayo nyumbani kisha alimwonyesha. Hta mama mmoja kwenye misa ya mchana alionwa na watu akichukua Ekaristi paada ya kupewa na kukimbia nayo mara tu baada ya misa.

Hivyo tujitahidi sana kuepuka kuendelea kupokea kwa mkono. MUNGU siyo shemeji yetu hadi tufikie hatua hiyo.

Tunaagizwa kupokea Ekaristi Takatifu katika hali ya neema. Hiki ni chakula lakini si chakula cha kawaida tu. Kwa kutokujali wengi wanapokea Ekaristi Takatifu bila kuwa katika hali ya neema ya utakaso. Ni kufuru ni sawasawa na kuandaa chakula vizuri na kwenda kukilia chakula hicho chooni. Ni heri usiisogelee Ekaristi Takatifu tusipokuwa katika hali ya neema ya utakaso. MUNGU hawezi kuchezewa na kiumbe awaye yote. Kama vile usivyoweka kidole chako kwenye moto, ukiogopa kuungua vivyo hivyo kwa Mwenyezi MUNGU.

Muujiza wa Lanciano – Italy 700
Mwujiza huu ulitokea kwa padre mmoja wa Shirika la Mt. Basili ambaye alikuwa na mashaka sana na mkate kugeuka kuwa mwili wa YESU na divai kuwa Damu ya YESU. Siku moja akiwa anaadhimisha ibada muujiza huo ulitokea na alijishtukia akipiga kelele; Nyama!!! Damu!!! Wanasayansi walipima na pasipo mashaka walihakikisha kabisa kwamba kweli ilikuwa nyama na damu ya mwanadamu. Hadi leo vipo. Tena ile damu imeganda katika vipande vitano kwa ukubwa na umbo tofauti lakini kila kibonge kimoja uzito wake ni sawa sawa na vyote ukipima kwa pamoja!!!!!!!!!!!!!
Wito ni kwamba tupokee Ekaristi Takatifu tukiwa katika neema ya utakaso na ikiwezekana tukiwa tumepiga magoti mdomoni. Endapo tutakuwa tunapokea tukiwa tumesimama, ni vema tuoneshe ishara ya heshima kwa Ekaristi Takatifu kwa kufunga mikono na kuinama kisha kupokea, au kupiga goti kisha kisimama na kupokea.
ZAKA NA SADAKA

“Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.” (1Kor 4:1-2)

Kuna mambo matatu yanayoonekana katika 1Kor 4:1-2.
1. Sisi tu watumishi wa Kristo. 1Kor 4:1ab.
2. Sisi tu mawakili wa siri za Mungu. 1Kor 4:1c.
3. Katika uwakili tunatakiwa kuwa waaminifu. 1Kor 4:2ab.

Utumishi.

Mtumishi ni nani? Mtumishi ni mtu anayemtumikia mwingine au ni mfanyakazi wa mtu mwingine. Kwa hiyo, Neno la Mungu linapotuita sisi “watumishi” maana yake kuwa sisi ni watu wa kumtumikia Yesu Kristo. Sisi ni wafanyakazi wa Yesu Kristo. Kwa kawaida utumishi au ufanyakazi ni kwa kupata malipo. Kwa hiyo, katika utumishi wetu kwa Kristo, yapo malipo. Kuna malipo. Hivyo hatumtumikii Kristo bure. Hatutwangi maji kwenye kinu, au hatupotezi kuni zetu katika kuchochea mawe. Hapana. Kuna mshahara, kuna malipo, yaani kuwepo pale alipo.

Katika makala haya tutaona yale mambo mawili ya mwisho katika 1Kor 4:1-2, yaani, mawakili wa siri za Mungu na uaminifu.

1. Wakili au mawakili.

Mawakili ni sawasawa na kusema “Wawakilishi”. Wakili ni “Mwakilishi”. Mwakilishi ni mtu anyesimama badala ya. Kwa hiyo, sisi tunaitwa mawakili wa siri za Mungu, maana yake, Mungu ameweka siri zake mikononi mwetu. Ametushirikisha katika siri zake.

2. Uaminifu.

Uaminifu kama lilivyotumika katika 1Kor. 4:1-2, maana yake ni kufanya sawasawa kama anavyotaka yule tunaye mwakilisha ambaye si mwingine bali ni Mungu. Mungu ametushirikisha siri zake na anatutaka tuwe waaminifu. Uaminifu katika mambo mawili. Jambo la kwanza, ni sisi wenyewe kuziishi siri hizo, yaani kuzifanyia kazi. Jambo la pili, wakati sisi tunapoziishi siri hizo, tunalazimika kuwashirikisha wengine waweze kuziishi siri hizo. Cha kushangaza zaidi ni kwamba uwakili huu, Mungu hakumpa malaika, bali ametupa sisi wanadamu.

Pamoja na kutuweka kwenye uwakilishi wa siri zake, bado Mungu huyo, ametupendelea sisi kwa kutupa uwakili huu wa mali zake. Kwa nguvu za Roho Mtakatifu, uwakili huu ulimshangaza sana mwimba zaburi mpaka akasema maneno haya; “Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; umemvika taji ya utukufu na heshima; umemtawaza juu ya kazi ya mikono yako; umevitia vitu vyote chini ya miguu yake. Kondoo, na ng’ombe wote pia; naam, na wanyama wa kondeni; ndege wa angani, na samaki wa baharini; na kila kipitacho njia za baharini.” (Zab 8:4-8).

Mungu ndiye muumbaji, na Mungu ndiye mwenye vitu vyote tunavyoviona na tusivyo viona. Hapa ametutolea mfano wa kondoo, ng’ombe, na wanyama wengine, na viumbe vyote vya baharini. Lakini hivyo vyote, Mungu ameviweka chini ya uwakili wa binadamu. Chini ya uwakili wa wewe na mimi.

Hebu tujiulize swali; Hivi, tumewahi kutulia na kutafakari kuwa mali zote tulizo nazo ni mali ya Mungu? Kama hujajua ukweli huu, utajulishwa; na kama ulikuwa unajua, sasa tuthibitishe kwamba mali zote ulizo nazo si zako wewe bali ni za Mungu. Na tumsikilize Mungu mwenyewe anavyosema katika Neno lake; “Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa Majeshi.” (Hag 2:8). Maana yake, fedha zote tulizo nazo mifukoni mwetu sasa hivi, zilizoko benki, tulizowakopesha watu, na dhahabu zote ni mali ya Mungu. Hata hizo pete, hereni, bangili na mikufu ya dhahabu zote ni mali ya Mungu.

Mungu anasema tena hivi; “Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako, wala beberu katika mazizi yako maana kila hayawani ni wangu na makundi juu ya milima elfu. Nawajua ndege wote wa milima na wanyama wote wa mashamba ni wangu. Kama ningekuwa na njaa singekuambia, maana ulimwengu ni wangu, navyo viujazavyo.” (Zab 50:9-12).

Hapa Mungu anasema, wanyama wote ni mali yake, na kama angekuwa na njaa asingekuambia wewe maana vyote ni vyake. Ng’ombe tulio nao, kondoo tulio nao, punda tulio nao, ngamia tulio nao, mbuzi tulio nao, sungura tulio nao, nguruwe tulio nao, ni mali ya Mungu. Pamoja na kuku na mayai yake, bata, njiwa ni mali ya Mungu.

Mungu anaendelea kusema; “Bwana asipoijenga nyumba waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji yeye aulindaye akesha bure.” (Zab 127:1). Nini maana yake? Maana yake ni kwamba, hata majumba tuliyo nayo ni mali yake. Maana kama Yeye asingejenga, sisi tusingekuwa na majumba hayo, na bado ni yeye anayeyalinda majumba hayo. Yeye ndiye anayelinda mali hizi tulizo nazo. Hii ni kusisitiza kuwa, vyote tulivyo navyo vimetoka kwa Mungu na bado vipo chini ya uangalizi wa Mungu. Ndiye anayevitunza na kuvilinda. Hii ni pamoja na uzima wako na afya yako.

Sasa huenda tunazidi kuelewa kuwa mali zote tulizo nazo ni mali ya Mungu. Swali linakuja; Je, nikwa nini sasa Mungu ametupa uwakili wa mali zake? Bwana Mungu ametupa sisi uwakili wa mali zake kwa sababu ya pamoja na hizi zifuatazo:

1. Sababu ya kwanza ni upendo wa Mungu kwetu Mungu anatupenda sana.
2. Pamoja na kutupenda kama tulivyo, bado pia Bwana Mungu anataka sisi tumtolee hizi mali zetu, na ndio maana Neno la Mungu linasema hivi; “Mheshimu Bwana kwa mali yako na kwa amlimbuko ya mazao yako yote.” (Meth 3:9)

Hebu na tujiulize maswali na kuyajibu mioyoni mwetu. Hivi sisi/mimi ni wakili mwaminifu? Je, ni wakili ambaye ninatumia mali za Bwana sawasawa na makusudi ya Mungu? Au, je, mimi ni wakili mbadhirifu? Wakili mchoyo? Wakili mbinafsi?

Ukweli ni kwamba wengi wetu si mawakili waaminifu. Ni mawakili wenye choyo na tumekuwa au hatumtolei Bwana kabisa au tumekuwa tukimtolea yale ambayo ni sehemu ndogo sana ya mali zetu.

Hebu tumsikilize Mungu mwenyewe anavyosema. “Tokea siku za Baba zenu, mmegeuka upande mkayaacha maagizo yangu wala hamkuyashika. Nirudieni mimi nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, turudi kwa namna gani? Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, tumekuibia kwa namana gani? Mmeniibia zaka na dhabihu (sadaka). Ninyi mmelaaniwa kwa laana, maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote.” (Mal 3:7-9); yaani wale wote wasiotoa zaka na sadaka, wamelaaniwa kwa maana wanamuibia Mungu.

Mungu anatuambia sisi kwamba tunaendelea kufanya yaleyale ambayo baba zetu waliyafanya. Maana hatutimizi maagizo yake. Baba zetu hawakutimiza maagizo ya Mungu, na sisi pia. Badala ya kubadilika, tunaendeleza moto ule ule wa wazazi wetu. Hatuyatimizi maagizo ya Mungu. Kutokana na kutotimiza maagizo yake, Mungu anasema tumrudie ili naye aturudie sisi. (Mal 3:7).

Kitu cha pili, anachosema Mungu katika Mal 3:7-9, ni kwamba anashangaa mwanadamu kumuibia Mungu. Mungu anashangaa maana kitendo cha mwanadamu kumuibia, sio tu kitendo kisicho faa, bali ni kitendo cha kutisha. Kitendo hicho kinatisha kiasi kwamba hata sisi wanadamu wenyewe tumeshikwa na mshangao hee! Mungu, tumekuibia kwa namana gani? Mungu anatuambia; “Mmeniibia zaka na sadaka.” (Mal 3:8)

Jambo la tatu, ambalo Mungu anaendelea kutuambia sisi wanadamu ambao tu mawakili wa mali zake katika Mal 3:7-9, ni kwamba; “Ninyi mmelaaniwa kwa laana maana mnaniibia mimi.” Wote ambao hatutoi zaka na sadaka tumelaaniwa kwa laana, maana ni wezi, kwani tunamuibia Mungu. (Mal 3:9).

Mungu anataka tumtolee zaka na sadaka. Haishii hapo tu kwa kutaka tumtolee zaka na sadaka, bali anatuambia waziwazi kwamba tusipotoa zaka na sadaka sisi ni wezi. Haishii hapo tu kwa sisi kubaki tu kwenye wizi bali tunalaaniwa, yaani tunpata laana. Hapa ni vema tuelewe vizuri, sio kwamba, tusipotoa zaka na sadaka Mungu atatulaani, la hasha. Isipokuwa kile kitendo chenyewe cha kutotoa zaka na sadaka, ni kibali tosha cha kutupatia laana. Mungu ndiye anayesema maneno haya.

Zaka na sadaka.

Maana ya zaka na sadaka na kazi zake.
Zaka.
Zaka ni kiwango maalumu kawaida ni 10%, ambacho wakili, yaani kila mmoja wetu, anapaswa kumtolea Mungu kutokana na mapato yake yote. Iwe ni pato la saa moja, siku moja, wiki moja, mwezi moja, au mwaka moja. Ni kiwango maalumu, 10%. Ni kama kodi.

Katika Agano la Kale, watu walikuwa hawaruhusiwi kuanza kutumia mapato yao yawe ya mashambani, ya wanyama, au fedha au dhahabu mpaka kwanza wametoa zaka. Na katika Agano la Kale, zaka hiyo ilikuwa ni asilimia kumi. (10%). “Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wanaamri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani ndugu zao kwa agizo la sheria, ijapokuwa wametoka katika viuno vya Ibrahimu.” (Ebr 7:5). Hiyo asilimia kumi walikuwa wamepewa Walawi wale ambao baadaye walikuwa makuhani, au waliokuwa wafanyakazi katika hekalu, katika Hema ya Bwana. Zaka zilikuwa zikitolewa kwa ajili ya hawa Walawi.

Katika makabila 12 ya Waisraeli, 11 yalikuwa na urithi. Lakini hawa Walawi, urithi wao ulikuwa Bwana mwenyewe pamoja na zaka na sadaka. Kila muisraeli alilazimika kutoa asilimia 10 ya mapato yake yote na kupeleka kwa hawa Walawi.

Kwa vile zaka ni mali ya Bwana, kila mtu alilazimika kutoa zaka bila kukosa. Ikiwa mtu angeshindwa kulipa zaka kutokana na sababu yeyote ile, mtu yule alipaswa kuifidia zaka ile kwa kutoa kile kiwango cha asilimia kumi na juu yake angeongeza tena asilimia 5. (Walawi 27:31). Zaka haikuwa kitu cha mchezo mchezo. Ilikuwa ni lazima. Mtu alikuwa na haki ya kutumia mali zake baada tu ya mtu huyo kutoa zaka, wala sio kabla ya hapo. Je, wewe unafanya hivyo? Hii inamaana hata sisi tusingeanza kutumia mishahara au mapato yetu mpaka kwanza tuwe tumetoa zaka. Hivyo ndivyo linavyoagiza Neno la Mungu.

Sadaka.

Kuna sadaka za aina tatu;
1. Sadaka za shukrani: “Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru, mtimizie aliye juu nadhiri zako.” (Zab 50:14)
2. Sadaka za wahitaji: yaani masikini. (Mdo 3:1-3)
3. Sadaka za sifa: “Basi kwa ajili yake Yeye (Yesu) na tumpe Mungu dhabihu za sifa daima yaani tunda la midomo iiungamayo jina lake.” (Ebr 13:15)
Nini maana za sadaka ya sifa? Sadaka za sifa ni pale ambapo mtu unakabiliwa na mambo magumu, mambo ya kukatisha tamaa, lakini bado unaweza kumsifu Mungu. Mfano ni ule wa yale yaliyomsibu Ayubu. Ayubu baada ya kufiwa na watoto wake wote na kupoteza mali zake zote, lakini bado alibaki akimsifu Mungu akisema; “Bwana ndiye aliyetoa, na yeye amechukuwa, jina la Bana libarikiwe.” (Ayu 1:21).

Mfano mwingine ni ule wa Paulo na Sila. Walikamatwa, walipigwa na walitiwa gerezani. Wakati wakiwa gerezani huku miili ikiwauma kutokana na mapigo, wakiwa wamekata tamaa kama vile Mungu wao hayupo, usiku walianza kumsifu Mungu. Waliimba na kumsifu Mungu huku wafungwa wengine wakiwashangaa kwani ilikuwa si kitu cha rahisi. “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wanamuomba Mungu na kumuimbia nyimbo za kumsifu na afungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.” (Mdo 16:25). Baadaye milango ya gereza ilifunguka, na aliachiwa.

Sadaka zitakazo elezewa katika makala hii ni sadaka za Shukrani. Zab. 50:14.

Kazi ya Zaka na Sadaka.

Zaka na sadaka ni za muhimu sana kwani kupitia Zaka na Sadaka ndipo Habari Njema za ufalme wa Mungu zimetangazwa na kuendelezwa hapa duniani sawasawa na maagizo ya Bwana Yesu aliyotuagiza akisema, “Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka. Asiye amini atahukumiwa.” (Mk 16:15-16).

Wengi wa waamini wanayo mawazo potofu na kusema si kazi yao ya kutoa zaka na sadaka bali ni kazi ya wazungu. Itikadi hiyo ni ya kizamani na imepitwa na wakati. Wengi wanaotoa zaka na sadaka kule ulaya ni wakulima na wafanyakazi wa kawaida kama wengi wetu tulivyo. Lakini wamegundua kuwa mishahara yao na mali zao ni mali za Mungu. Wameamua kutoa zaka na sadaka hadi Injili ikatufikia. Mbali na kuifanya Injili ienee duniani, zaka na sadaka hutumika katika kulitegemeza kanisa kwa kuleta maendeleo ya kimwili na ya kiroho kwa watu. Kwa mantiki hiyo, ni lazima kutoa zaka na sadaka.

Kulingana na Mal. 3:8, wale wote wasiotoa zaka na sadaka ni wezi. Wizi upo wa aina mbili. Wizi wa kwanza ni ule wa kuiba kidogokidogo, yaani kudokoadokoa. Mfano, kuna mtu kaweka gunia lake la mahindi sehemu fulani, na wewe unaenda kuiba kidogokidogo, leo debe, kesho kilo40, keshokutwa debe mbili hadi guia lote linaisha. Wizi wa aina ya pili ni ule wa kuiba jumla. Mfano, mtu ameweka gunia lake la mahindi pale, na wewe unaenda kulibeba lote na kuondoka nalo. Hivyo basi, mtu akiwa anaiba kidogokidogo au jumla, ni mwizi tu, kwani wizi ni wizi tu.

Hata katika kumuibia Mungu tupo wezi wa aina mbili. Kuna wezi wanaomuibia Mungu kidogokidogo, yaani wanatoa zaka na sadaka kiduchu. Wenyewe wanaona inatosha bwana. Mfano, mtu anazo shilingi elfu mbili, anachenji ili atoe shilingi mia na zilizobakiza mfukoni atazitumia kwa kunywea pombe mara atokapo kanisani. Kwa jinsi hiyo, wewe ni mwizi.

Mwingine hatoi kabisa huku akijipa moyo kwa kujidanganya kwa maneno mbalimbali pamoja na haya yafuatayo. Utasikia mtu akisema hivi; “Aah bwana wee, hata hii sadaka au zaka hii kidogo natoa kwa basi tu. Kwanza Paroko wetu ananikwaza sana. Pesa zetu tunazo mpa anasaidia ndugu zake. Kwanza ashukuru hata hiki kidogo ninachotoa.”

Ukweli ni kwamba kwa suala la kutoa sadaka na zaka si suala la paroko au padre fulani. Sio suala la hiari bali ni suala la lazima. Ni Mungu anayetaka wewe utoe zaka na sadaka. Anatutaka tutoe zaka na sadaka kwa sababu yeye ndiye aliyetupa vitu hivyo. Ni kwa sababu hiyo. Ametupa wanyama, mishahara, majumba, mali na vitu vingine vya thamani ili tumtolee zaka na sadaka. Hivyo, hatuna sababu yeyote ya msingi ya kutokutoa zaka na sadaka.

Mwingine utamsikia akisema “Aah bwana wee, mimi sitoi sadaka wala zaka. Kisa? Kwanza mshahara wangu ni mdogo. Hautoshi mimi na mke wangu wala na watoto wangu. Sasa nitatoaje zaka na sadaka?”

Ndugu zangu, hebu tuyasikie maneno ya Mungu; “Aliye muaminifu katika lililo dogo sana, huwaminifu katika lililo kubwa pia. Na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.” (Lk 16:10). Mfano, ikiwa katika mshahara wako wa sasa wa shilingi 30,000/= unashindwa kutoa zaka ya Sh. 3,000/= kwa mwezi, Mungu gani atakayekupa wewe mshahara wa Sh. 500,000/= ili baadae umtolee zaka ya Sh. 50,000/= kwa kila mwezi, wakati wewe unashindwa kutoa Sh. 3,000/= katika mshahara wako wa Sh. 30,000/=? Haiwezekani. Ndiyo maana Mungu amekudhibiti, huwezi kupata mshahara mkubwa. Na hupati ng’o.

Kazi ya zaka ni kufungua baraka za mbinguni. (Mal. 3:10) Milango ya mibaraka ya mbinguni inafunguliwa na zaka na sadaka tunazotoa. Kwa vile wewe hutoi zaka, huwezi kubarikiwa. Hutapata mshahara mkubwa, hutapata pato la kutosha. Utabaki hapohapo ulipo, na kuendelea kulalamika tu kila siku. Maana wewe ni mchoyo.

Mfano, wazazi wanaweza kujua kwamba mtoto wao fulani atakapokuwa mkubwa hawezi kutunza fedha, hasa kutokana na matumizi ya fedha ndogondogo wanazompa mtoto wao. Mathalani, wamempa mtoto wao Sh. 2000/= kwa matumizi ya wiki, eti baada ya siku mbili anakuja na kulalamika kuwa ile hela imeisha. Unampa hela nyingine na baada ya siku moja anakuja tena akilalamika tena. Hii inonyesha jinsi mtoto asivyoweza kutunza fedha, na hata akiwa mkubwa hali itakuwa ni hiyo hiyo, kwani atakuwa mbadhilifu.

Na Mungu ni hivyo hivyo. Kesha kujua wewe kutokana na mshahara wako wa Sh. 30,000/= ambao unaupata sasa hivi, na kushindwa kumtolea zaka na sadaka. Kesha kujua wewe ni mchoyo na anauhakika akikupa Sh. 1,000,000/= huwezi na hutakuwa tayari kutoa laki moja kama sehemu yako ya zaka kwa kila mwezi. Kwa hivyo unabaki kama ulivyo. Kila siku njaa, kila siku tabu, kila siku madeni, kila siku malalamiko na kila siku kukosa amani. Sababu yenyewe mshahara mdogo. Hiyo ndiyo laana ya ufukara. Ndugu, tusipotoa zaka na sadaka, tunapata laana, na laana yenyewe ni ufukara.

Mungu kwa kinywa cha nabii Hagai anatuambia; “Ninyi msiotoa zaka na sadaka, mtapanda mbegu nyingi, mtavuna kidogo. Mtakula lakini hamtashiba, mtakunywa lakini hamtajazwa na vinywaji. Mtajivika nguo lakini hamtapata joto, na yeye atakayepata mshahara atapata mshahara ili autie kwenye mfuko uliotobokatoboka.” (Hag 1:6)

Ndugu yangu, unalalamika mshahara hautoshi, au pato unalopata halitoshi, ndio! Unalalamika njaa, ndio! Unalalamika unapanda kwa wingi na kupata kidogo, ndio! Hiyo ni laana ya ufukara, kwa sababu hutaki kumtolea Mungu. Tunamuibia Mungu zaka na sadaka. Neno la Mungu linasema hivyo.

Hivyo, kama bado hujafunguka kwa kumtolea Mungu zaka na sadaka kwa kujisingizia au kujibandikizia vijisababu visivyo vya msingi pamoja na kwamba pato lako ni kidogo. Mungu hatokubariki zaidi ya hapo ulipo mpaka umeanza kuwa muaminifu. Maana kama katika Sh. 1,000/= unashindwa kumpa Sh. 100/= kwa kila mwezi, amini Mungu hatokupa 100,000/= kwa sababu anajua hutakuwa tayari kumtolea Sh. 10,000/= kwa kila mwezi. Mwenye akili timamu anajua ukweli huo.

Na wewe ndugu yangu unayesema, “mimi sitoi zaka na sadaka, ninatoa kidogo tu eti kwa sababu paroko ananikwaza, eti matumizi yake siyapendi sijui nini na nini”, hebu sikiziliza Mungu anavyokuambia sasa. “Msihukumu msije mkahukumiwa, kwakuwa hukumu ile muhukumuyo ndiyo mtakayo hukumiwa, na kipimo kile mpimiacho, ndicho, mtakacho pimiwa.” (Mt. 7:1-2). Usiache kutoa zaka eti unakwazwa na matumizi ya paroko au padre fulani, la hasha. Neno lina sema usihukumu usije ukahukumiwa, pili, kipimo kile mpimiacho ndicho mtakachopimiwa. Ndiyo maana baraka, mapato katika nyumba yako yamepungua. Unahangaika, umekata tamaa maana kile unachopimia ndicho Mungu anachokupimia.

Yesu kama Mungu, kwa vile ilikuwa ni sehemu ya sheria, naye alitoa zaka na sadaka. Ikiwa huyu Yesu tunayemfuata, tayari ametoa zaka na sadaka, wewe ni nani ushindwe na hata ukatae kutoa zaka na sadaka? Yesu na mitume walitoa zaka na sadaka. (Mt 17:24-27). Hivyo, narudia tena kwa kusema, tusipotoa zaka na sadaka, sisi ni wezi na tunapokea laana ya ufukara.

KANUNI ZA MSINGI ZA UTOAJI WA KIKRISTO

Kwa kuwa utoaji wa kweli wa Kikristo unatokana na neema ya Mungu ambayo ni lazima kuiomba, neema itendayo kazi ndani ya muumini, ni wazi kwamba utoaji wa kweli wa Kikristo hububujika kutokana na uhusiano mwema wa mtu na Mungu. Wakristo wa Mekadonia (2 Kor. 8:12), walikuwa katika njia sahihi maana, ”……kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana…” Mambo mengine yote yanatokana na hatua hii.

Zifuatazo ni kanuni nyingine mbili zisizo epukika:

Kwanza, ni lazima kuwepo na NIA YA HIARI. (2 Kor. 8:12). Nia ya hiari husababish kutoa kwa ukunjufu wa moyo ambako ndiko Mungu apendako. “Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.” (2 Kor 9:7). Kutoa bila maning’uniko, kinyongo, au kulazimishwa ikiwa kuna NIA ya HIARI. Utoaji uwe wa furaha siyo mzigo. Utayari wa NIA hufanya tendo la utoaji liwe la ibada ya kweli.

Pili, Paulo mtume, anatamka kwamba penye nia ya hiari “hukubaliwa kwa kadiri ya alivyonavyo mtu, si kwa kadiri asivyonavyo.” Utoaji wa kadiri ya uwezo wa mtu ni kanuni inayofundishwa katika Biblia nzima. Ndiyo maana utoaji wa fungu la kumi ni njia bora ya utoaji; inafanya mzigo ubebwe kwa usawa. Mungu hupokea kile kilichotolewa kwa roho safi ikiwa kimetolewa kulingana na uwezo wa mtu.

Ukweli huu unathibitishwa na tendo la Yesu kumsifia yule mjane ambaye akiweka sarafu ndogo mbili katika sanduku la sadaka. (Mk 12:42-44). Mbele ya Yesu, huyu mjane alitoa zaidi ya wale matajiri ambao wameleta fedha nyingi za ziada. Ila yule majane aliweka fedha zote alizokuwa nazo. MUNGU HAANGALII KIASI KILICHOTOLEWA BALI KILE KILICHOSALIA.

Katika 2 Kor 9:6, Mtume Paulo anatumia kanuni ya kulima ambayo inafanana na utoaji wa Kikristo. Mkulima apandaye mbegu kidogo, hawezi kutarajia mavuno makubwa. Ni pale apandapo mbegu za kutosha, na ikiwa hali ni nzuri, anaweza kutarajia mavuno tele. Kwa njia hiyo hiyo, Mtume Paulo anasema muumini anapotoa kulingana na alivyo navyo, na akifanya hivyo kwa moyo mkunjufu kwa Mungu, kile atoacho kinakuwa kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo. Haitaonekana tena bali kutokana na hiyo mbegu, mavuno yatachipuka kulingana na mbegu zilizopandwa.

Wakulima ni wenye hekima kuliko wakristo wengi. Hata kunapokuwa na upungufu wa chakula, wao wanapanda mbegu kwani wanajua kwamba pasipo kupanda, hakuna kuvuna. Lazima ieleweke kwamba hatupaswi kutoa ili tupate. Nia kama hiyo haikubaliki mbele za Mungu. Tunatoa kwa sababu ni haki kutoa. Mungu ndiye asitawishaye mavuno. Tunamwachia yeye matokeo. Baraka ya Mungu ni zaidi ya fedha na inaenea katika sehemu zote za maisha yetu.

NEEMA YA KUTOA

Mungu anataka watu wake wabarikiwe kwa njia ya kutoa. Lakini inawezekana kutoa bila kupata baraka kwa sababu NIA ni ya muhimu, na Mungu anatazama moyo.
§ Utoaji usio mpendeza Mungu;
1. Kutoa kwa nia ya kujionyesha kwa watu (Mt.6:1-4)
2. Kutoa kwa huzuni (2 Kor. 9:7)
3. Kutoa kisheria (Mt. 23:23)
4. Kutoa ili kupata (Efe 6:1)
5. Kutoa kidogo kuliko pato lako halisi (Mt. 12:42-44)

§ Utoaji unaompendeza Mungu:
1. Kutambua kwamba vyote tulivyonavyo vyatoka kwake (1 Nya. 29:14)
2. Kumtolea Mungu
3. Kutoa kwa furaha toka moyoni. (2 Kor. 9:7)
4. Kutoa kwa ukarimu, kadiri Bwana alivyokufanikisha. (Rum. 12:8)

HITIMISHO.

Baada ya kusoma kwa makini haya yote, Mungu mwema, mabaye anataka sasa uanze maisha mapya, anakuomba sana kuanza kufanya toba ya dhati endapo kwa muda mrefu hukuwa unatoa zaka na sadaka inavyostahili kwa Mungu. Toba hii ihitimishwe kwa kupokea vema na sahihi na kwa ibada sakramenti ya Kitubio ili kupata msamaha wa Mungu. Mungu atakusamehe makosa yako yote na kusahau dhambi zako zote, na hivyo kukupatia neema ya utakaso na kuwa kiumbe kipya na kuanza sasa maisha mapya. Baada ya hapo, anza sasa bila kuchelewa kutoa zaka na sadaka kwa UAMINIFU WAKO WOTE, TENA KWA FURAHA BILA HUZUNI WALA KUREGEA TENA.

Mungu anatuambia kwa kinywa cha Mt. Paulo; “Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu.” (1 Tim. 6:7), Ayubu anaongezea kwa kusema; “Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko nili uchi vile vile.” (Ayu. 1:21). Ukweli huu unadhihirishwa na maneno yafuatayo; “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni..” (Fil 3:20). Kristu anatutahadharisha akisema; “Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake?” (Mt. 16:26). Dunia na fahari yake yote itapita, lakini Neno la Bwana halitapita. Angalia usiwe unajiwekea hazina duniani na kuja kuambiwa kama alivyoambiwa tajiri mpumbavu “ Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?” (Lk. 12:20).

SIFA NA UTUKUFU NI KWA MUNGU. ALELUYA