Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), imeingia makubaliano ya kupeleka marubani wake kufundisha na kusimamia ndege mpya za Airbus A220 za Kampuni ya Ndege ya Ibom iliyopo nchini Nigeria.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mha. Ladislaus Matindi, amethibitisha kuwepo kwa makubaliano hayo ambapo amesema ATCL imetoa marubani wake waandamizi wawili ambao watakuwa na jukumu la kuwafundisha kwa vitendo marubani na walimu wa marubani wa Ibom Air kwa muda wa miezi sita.

"Marubani wa ATCL watakuwa na jukumu la kufundisha na kusimamia mafunzo kwa vitendo hadi watakapojiridhisha kuwa marubani wanafunzi na walimu wao wamefikia viwango vinavyotakiwa kurusha ndege hizo", alisema Mha. Matindi.

Aidha, Kampuni ya Ibom Air itailipa ATCL gharama za mafunzo hayo kwa mujibu wa mkataba kwa kipindi chote cha makubaliano.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya ATCL kuonesha uzoefu wa muda mrefu wa kumiliki ndege za Airbus A220-300 na pia kuridhishwa na kiwango cha umahiri wa marubani wa Air Tanzania.

Mafunzo hayo yanalenga kujenga uwezo kwa marubani wa Ibom Air watakaorusha ndege za Airbus A220, ambazo ATCL ina uzoefu wa miaka mingi wa kumiliki ukilinganisha na Ibom Air ambao ndio wanaanza kutumia ndege za aina hiyo.

ATCL ina zaidi ya marubani 100 na inamiliki ndege aina ya Boeing B787-8, B737 MAX 9, B767-300F, Airbus A220-300 pamoja na Dehaviland Q400 na Q300.
Marubani waandamizi wa Kampuni ya Ndege Tanzania Kept. Sajjad Moloo na
Kept. Arif Jinnah (kulia na kushoto) wakiwa ndani ya ndege kwa ajili ya mafunzo kwa walimu na marubani wa ndege ya Ibom, nchini Nigeria




Marubani waandamizi wa Kampuni ya Ndege Tanzania Kept. Sajjad Moloo na
Kept. Arif Jinnah (kulia na kushoto) wakiwa ndani ya ndege kwa ajili ya mafunzo kwa walimu na marubani wa ndege ya Ibom, nchini Nigeria
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo pamoja na Wataalam wengine wamesili katika Mji mdogo wa kilwa kivinje wilaya Kilwa mkoani Lindi kwa usafiri wa boti kutoka Somanga kupitia baharini kwa ajili ya kuangalia hali Miundombinu na kuwafikia Wananchi kutokana na mawasiliano ya Barabara ya Lindi – Dar- es Salaam kukatika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zilizoambatana na kimbunga Hidaya, leo tarehe 05 Mei 2024.






Na. Dennis Gondwe, KIWANJA CHA NDEGE

WANANCHI wa Mtaa wa Osterbay, Kata ya Kiwanja cha Ndege Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamejitokeza kufanya usafi wa mazingira katika eneo la Shule ya Msingi Mlimwa B kwa lengo la kuweka mazingira safi na kuepuka na magonjwa ya mlipuko kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mtendaji Mtaa wa Osterbay, Ashura Iberia alipokuwa akiongea na wananchi wa Mtaa wa Osterbay waliojitokeza kwa wingi kufanya usafi wa mazingira katika Shule ya Msingi Mlimwa B.

Iberia alisema “leo tumefanya usafi wa mazingira kuzunguka Shule ya Msingi Mlimwa B, wananchi wa Mtaa wa Osterbay wamejitokeza kwa wingi kufanya usafi wa mazingira. 

Lengo la kufanya usafi huo ni kuweka mazingira ya shule safi ili wanafunzi ambao ni watoto wetu wasome katika mazingira safi na salama. Lakini pia kuwaepusha wanafunzi na jamii inayozunguka shule hii na magonjwa ya mlipuko. Zoezi hili nimelisimamia mimi mwenyewe Afisa Mtendaji Mtaa wa Osterbay ili kutoa chachu na hamasa kwa usafi wa mazingira kwa kila mwananchi”.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa wa Osterbay, Hussein Ngura alisema kuwa kuanzia siku hiyo usafi ni agenda ya mtaa. “Kuanzia leo agenda yetu kuu ya Mtaa wa Ostebay ni usafi wa mazingira kama alivyosema Afisa Mtendaji wa Mtaa. Kama tutakumbuka aliwahi kufika hapa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma na kukagua usafi kwa kustukiza. 

Sasa hatujui ni kiongozi gani atafuata kuja kukagua, hivyo lazima tujipange kwa kuweka mazingira yetu safi. Wananchi wa Mtaa wa Osterbay mmenitendea imani kuwa nina watu kwa jinsi mlivyojitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hili la usafi wa mazingira. Pia, mimi namsifu sana Afisa Mtendaji wa Mtaa wetu kwa kazi nzuri anayofanya, hakika ni mchapa kazi hodari na anatuongoza vizuri” alisema Ngura.

Zoezi la usafi wa mazingira katika Mtaa wa Osterbay, Kata ya Kiwanja cha Ndege liliongozwa na Afisa Mtendaji wa Mtaa, na kuhudhuriwa na wenyeviti, mabalozi na mamia ya wananchi.




Halmashauri ya mji wa Njombe mefanikiwa kutoa chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri kati ya 9 - 14 kwa 91% na kuvuka lengo la angalau 80% kitaifa huku wakitarajia kufikia 100% ifikapo Mwezi Disember 2024 mwaka huu ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Simon Ngassa ni mtaalamu wa afya ambaye ni mratibu wa chanjo wa halmashauri hiyo akizungumza na vyombo vya habari amesema licha ya changamoto kadhaa walizopitia katika zoezi hilo lakini wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa chanjo kwa mabinti wengi kupitia shuleni na mikutano ya hadhara baada ya elimu kutolewa.

"Halmashauri ya mji Njombe tumefanikiwa kufikia 91% na kuvuka lengo lile ambalo tulikuwa tumepewa angalau 80% kitaifa hivyo tunaendelea kutoa huduma,na hawa ambao wataendelea kupata kwenye utaratibu wa kawaida ni matarajio yetu inapofika mwezi Desember mwaka huu nao wataingia kukamilisha asilimia hizi ambazo zimebaki"amesema Ngassa

Aidha Ngassa amesema halmashauri bado ina chanjo za kutosha ambapo ametoa wito kwa walengwa kuendelea kufika kwenye vituo vya afya kwa ajili ya chanjo hiyo.

"Tunatoa wito kwa wazazi kwamba huduma hii ya kutoa chanjo inaendelea kwenye vituo vyetu kwa wasichana wale ambao hawakuweza kupata chanjo ili inapofika mwezi Disember wasichana wote wawe wamekingwa dhidi ya saratani ya mlano wa kizazi kwa hiyo chanjo zipo kwenye vituo vyote vya kutoa huduma za afya"aliongeza Ngassa




Na Fauzia Mussa Maelezo.05.05.2024.

Mkuu wa Oganaizesheni Afisi Kuu ya chama cha mapinduzi Zanzibar Omar Ibrahim Kilupi amezitaka jumuiya za chama cha Mapinduzi kuweka mikakati ya kuwatambua vijana ambao hawajasaliliwa katika datfari la wapiga kura ili waweze kusajiliwa.

Akifungua kongamano la jumuiya ya wazazi wa Mkoa wa Magharibi Kichama huko Skuli ya Ali Hassan Mwinyi Bububu amesema kuna baadhi ya vijana hawakujiandikisha katika awamu iliopita hivyo ni vyema kuwatambua na kuwahamasisha kujiandikisha katika awamu ijayo.

Amezitaja baadhi ya sababu zilizopelekea vijana hao kutojisajili kuwa ni pamoja na kutotimiza umri wa miaka 18 pamoja na kuwa mbali na vituo vya kujiandisha kwa kipindi hicho.

Aidha amezitaka jumuiya hizo, kuhakikisha vijana wote waliotimiza vigenzo wanajisajili ili kuweza kupata vijana wengi watakaoendelea kukiweka madarakani chama cha Mapinduzi ifikapo 2025.

“Kuna kundi la wananchi ambao wana sifa za kujisajili lakini hawajaenda kujisajili na kama tunavyojuwa kama hukujisajili katika daftari la kudumu la wapiga kura hutoweza kupiga kura, tuendeni tukahamasishe ili tusije kumuacha mtu nyuma.” alisema Kilupi.

Aidha amesema lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu ya uchaguzi na mmongonyoko wa maadili na kuwataka kuyafanyia kazi mafunzo walipopewa sambamba na kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao.

Kwa upande wake Mlezi wa Mkoa wa magharibi kichama ambae pia Mwakilishi wa viti maalum kupitia jumuiya ya wazazi mkoa wa kusini Unguja Mhe. Sabiha Filfil Thani amesema kuna kila sababu ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuendelea kubaki madarakani katika Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani kutokana na kutekeleza kwa vitendo ilani ya chama hicho.

“Ilani ya CCM ilimtaka rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kujenga madarasa 1,500 kwa Skuli za Unguja na Pemba ambapo amevunja rikodi kwa kujenga madarasa 2273 sawa na silimia 150 ya malengo ya ilani ya chama cha Mapinduzi.” amefahamisha Mlezi huyo.

Katika kongamano hilo mada mbili ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo mmongonyoko wa maadili na uchaguzi Mkuu ambapo Kauli mbiu ni ”USHINDI WA CCM 2024-2025 JUMUIYA YA WAZAZI TUPO MSTARI WA MBELE”







Na; Mwandishi Wetu – Songea

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe Jenista Mhagama amezindua Mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA) katika kijiji cha Mpitimbi kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini Mkoani Ruvuma Tarehe 4 Mei 2024.

Mradi huo wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA) unaoenda kutekelezwa katika Wilaya nne za Mikoa ya Ruvuma na Lindi, na kulenga katika kunufaisha kaya elfu Moja (1000) katika Wilaya za Songea vijijini, Mbinga Mkoani Ruvuma, Ruhangwa na Mtama Mkoani Lindi, ambapo pamoja na mambo mengine Familia na jamii hizo zinaenda kuinua hali ya maisha kwa kuongeza kipato na kuimalisha Lishe.

Akiongea katika uzinduzi wa mradi huo,Waziri Mhagama alisema Mpitimbi imebahatika kuanza na mradi huu, na kwakuwa Mkoa wa Ruvuma unaongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula lakini, una changamoto ya udumavu,”Na ndiyo maana Serikali imeleta mradi huu ambao utatumia takribani zaidi ya shilingi Bilioni tatu nukta moja, katika maeneo tuliyojipangia, ambao ni sehemu ndogo tuu ya Programu kubwa ya kuendeleza sekta ya Kilimo na Uvuvi, Tumebahatika kuanza na mradi huu unaofadhiliwa na ubalozi wa Norway Nchini hivyo ni wakati mzuri wa Wilaya zitakazonufaika kuweza kujikimu kimapato na kiafya.” Alisema.

Aliendelea kusema kuwa, kwa kuwa hali ya udumavu inaleta changamoto ya afya ya akili ni fursa sasa kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma kuendelea kuboresha afya, kupitia lishe ya viumbe maji na hasa Samaki.

Waziri Mhagama aliushukuru ubalozi wa Norway kupitia shirika lake la NORAD kuleta mradi huo mkoani Ruvuma, “Leo Tunazindua Shamba Darasa Ambalo linaenda kuchagiza maendeleo ya tabianzuri ya biashara na matumizi ya lishebora kupitia samaki wanaofugwa kwenye mabwawa, na miradi itakayofanywa kwenye baadhi ya halmashauri za Mkoa wa Ruvuma.” Alisisitiza.

Alibainisha kuwa, Kupitia bwawa kubwa la Asili lililopo Mpitimbi ni wakati sahihi sasa wa kuimarishwa kwa bwawa hilo na kuanza kwa ufugaji mkubwa wa Samaki “Tunatamani kuona kuwa Bwawa hilo lenye ukubwa wa hekari 17.4 linaendelezwa na kuwa shamba Darasa.” Alisema

Awali, Waziri Mhagama Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa, kupeleka Miradi mingi ya Maendeleo katika Mkoa wa Ruvuma.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa alisema, kupitia mradi huo unaoenda kutekelezwa kwa miaka miwili,Tanzania imekuwa Miongoni mwa nchi tatu za Afrika kupata bahati ya kunufaika na Mradi huo, zikiwemo nchi za Kenya na Msumbiji.

Aliendelea kusema kuwa, mradi huo wa kuendeleza Lishe na ufugaji endelevu wa viumbemaji na ukulima wa mwani kwa wakulima wadogo unatekelezwa katika mikoa kumi na moja ya Tanzani Bara pamoja visiwa vya unguja na Pemba.

Akiongea katika ghafla hiyo muwakilishi kutoka Mfuko wa Kimataifa wa maendeleo ya Kilimo nchini (IFAD) Bi. JacquiIine Machangu Motcho aamesema, IFAD imekuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika nyanja na sekta zinazolenga, kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta ya kilimo hususani Wakulima wadogo wadogo hasa wale walio vijijini.

Na aliendelea kusema kuwa, Shirika hilo limeendelea pia kuyapa kipaumbele maeneo hayo ikiwa na dhamira ya kuinua na kuboresha sekta ya Kilimo, Mazao, Mifugo na Uvuvi ili kufikia uzalishaji wa juu ulio endelevu na wenye faida kibishara, unaoleta ukuaji wa pamoja kiuchumi na Taifa zima kwa ujumla.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Bi JacquiIine alisema Kupitia Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi, IFAD imepokea ufadhili-ruzuku(grant) kwa mradi wa ARNSA kutoka Ubalozi wa Norway, unaolenga kupunguza umaskini na kuboresha lishe kupitia shughuli za Ufugaji wa Samaki wenye tija na ustahimilivu kutoka kwa wazalishaji/wafugaji wadogo. Dhamira yake ya kimaendeleo inalenga kuongeza mapato, kujenga ustahimilivu na kuwajengea uwezo kimaisha wafugaji wadogo wa samaki walio vijijini.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza katika Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa, akitoa Neno la Utangulizi wakati wa Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024

Picha ikionesha Baadhi ya washiriki wakati wa Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024
Muwakilishi kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo nchini (IFAD) Bi. JacquiIine Machangu Motcho, akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024
Aliyeinama, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama, akiweka mbegu ya Samaki katika moja ya Bwawa, wakati wa Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024


Picha ya pamoja Baadhi ya washiriki, baada ya Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024

Na Munir Shemweta, MLELE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Mhe, Geophrey Pinda amekabidhi gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Kibaoni.

Mhe, Pinda amekabidhi gari hiyo tarehe 4 Mei 2024 katika hafla maalum iliyofanyika eneo la Kibaoni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Mlele akiwemo Mkuu wa wilaya hiyo Alhaji Majid Mwanga na Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Daud.

Kukabidhiwa kwa gari hilo kunaifanya halmashauri ya Mpimbwe kuwa na jumla ya magari matatu ya kubebea wagonjwa yanayohudumia vituo vya afya vya Kibaoni na Usevya huku gari moja ikihudumia hospitali ya wilaya ya Tupindo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Pinda amewaomba wananchi wa kibaoni kuitumia gari hiyo kwa manufaa yao huku akimtaka mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe kuhakikisha gari waliyokabidhiwa inabakia kwa matumizi ya kituo hicho cha afya cha Kibaoni.

‘’Gari ya Kibaoni ikae kibaoni na kule Mamba nikuombe vile vile apatikani dereva haraka na akae pale gari inapolala kwa sababu magari haya siyo mapambo na ni huduma muhimu kwa wananchi’’ alisema Mhe, Pinda

Ameweka wazi kuwa, gari hilo linaenda kuongeza uwezo kwa kituo hicho cha afya kwa kuwa mtu akipata rufaa kutoka Kibaoni kwenda Hospitali ya wilaya mafuta hayatatumika sana tofauti na hapo awali ambapo ililazimika mgonjwa kupelekwa sumbawanga.

Upatikanaji gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Kibaoni kutasaidia kutatua changamoto za usafiri sambamba na kurahisisha huduma za dharura kwa maeneo jirani na hiyo inatokana na kuongezeka kwa mahitaji katika eneo la Kibaoni kama vile uwepo wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda.

Mhe, Pinda amewaeleza wananchi wa Kibaoni kuwa, gari iliyokabidhiwa ni mali yao na itatumika kwa kazi za dharura hasa wagonjwa na sasa hakutakuwa tena na ulazima wa kukodi bajaji kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa walio katika hali hatarishi na atabebwa na gari hiyo ku[elekwa mahali ambapo madaktari wamependekeza kupelekwa.

Wananchi wa Kibaoni wamemshukuru Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe, Geophrey Pinda kwa kusaidia upatikanaji wa gari hilo la wagonjwa pamoja na fedha za ujenzi wa kituo cha afya cha Kibaoni.

Kwa mujibu wa taarifa ya halmashauri ya Mpimbwe, mwezi Januari 2024 kituo hicho kilipokea shilingi milioni 175 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba pamoja na umaliziaji majengo ya Maabara, Jengo la Mama na Mtoto, Upasuaji na Kichomea Taka.

Ukamilishaji wa kituo cha Afya Kibaoni utatoa huduma kwa wananchi takriban 28,817 wa kata ya kibaoni na viunga vyake.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akikata utepe kuzindua gari la kubebea wagonjwa la Kituo cha afya cha Afya Kibaoni tarehe 4 Mei 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akimkabidhi fungua ya gari la wagonjwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi Shamim Daudi tarehe 4 Mei 2024.
Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Myumba na Maendeleo Mhe Geophrey Pinda (katikati), Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaji Majid Mwanga (aliyevaa tai), Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Daud (aliyenyoosha funguo) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpimbwe Silas Ilumba (kushoto) wakifurahia mara baada ya makabidhiano ya  gari la wagonjwa kwa ajili ya kituo cha Afya Kibaoni tarehe 4 Mei 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akizungumza na wananchi wa Kibaoni mara baada ya kukabidhi gari la wagonjwa kwa kituo cha afya kibaoni tarehe 4 Mei 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akiwaongoza viongozi wengine kwenda kukabidhi gari la wagonjwa kwa kituo cha Afya Kibaoni tarehe 4 Mei 2024.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameeleza kuwa timu ya watalaamu wa Wakala ya Barabara (TANROADS) na Makandarasi itatumia saa 72 (siku 3) kukamilisha zoezi la kurejesha miundombinu ya barabara ya Lindi – Dar es Salaam, ambayo imeharibiwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zilizombatana na kimbunga Hidaya.

Amesema hayo Mkoani Lindi Mei 05, 2024, mara baada ya kuwasili na kukagua uharibifu wa miundombinu ya barabara ya Lindi - Dar es Salaam na kuzungumza na wananchi na wasafiri wa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, na Dar es Salaam wanaotumia barabara hiyo na kutoa pole na kuwataka kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kujereshwa miundombinu.

“Mitambo ipo inaletwa hapa, kazi ya kurudisha mawasiliano ya barabara hii itaanza wakati wowote kuanzia sasa, ni lazima tuanze na kipande kimoja ili tuweze kufika katika maeneo mengine yaliyoathiriwa. Namna miundombinu imeharibika na tathmini iliyofanyika tunahitaji masaa yasiyopungua 72 ili kuweza kurudisha mawasiliano,” amefafanua Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa mawasiliano ya barabara hiyo yamekatika katika maeneo matano ambayo ni pamoja na eneo la barabara ya Somanga – Mtama, eneo la Mikereng’ende kutokea Somanga na eneo la Lingaula kutokea Lindi.

Aidha, Bashungwa amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itafanya kila jitihada ili ifikapo Jumatano jioni mawasiliano ya barabara hiyo yarejee katika hali yake.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo ameeleza kuwa maji yaliyokuwa yakipita juu ya barabara yalizidi kiwango na kusababisha madaraja kushindwa kuhimili wingi na kasi ya maji na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo matano ikiwemo Somanga, Mikereng’ende, na Lingaula.

Nyundo amemueleza Waziri Bashungwa kuwa kazi ya awali iliyofanyika ni kuwasiliana na taasisi zinazohusika kwa Mkoa wa Ruvuma, Mtwara na Lindi ili kutoa taarifa kwa wasafirishaji na watumiaji wa barabara hiyo kusimamia safari zao mpaka pale miundombinu itakaporejeshwa katika hali yake.








*Awashangaa kumchonganisha Rais Samia kwasababu tu ni Mzanzibar

*Apangua hoja Kuhusu madai Katiba mpya,Sheria mpya ya uchaguzi


Na Said Mwishehe, Dodoma


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ameshauri wananchi kutokubali hoja za kejeli, chuki na kugombanisha watu zinazotolewa na CHADEMA.

Pia Kinana amesema viongozi wa CHADEMA kwa katika mikutano yao ya hadhara wamekuwa wakieneza chuki na kumchanganisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa hoja dhaifu kwamba anatoka Zanzibar na amekuwa anaihujumu Bara.

Akizungumza leo Mei 5,2024 Wana CCM pamoja na wananchi alipokuwa katika mkutano maalumu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Kinana amesema CHADEMA katika mizunguko yao wameituhumu CCM, Serikali na Rais kwa hoja za uongo.

"Hatukatai kukoselewa, hatukatai kusahihishwa, lakini hatukubali kuzuliwa au kushutumiwa kwa mambo ambayo hayapo. Kubwa ambalo wamefanya ni kujenga chuki miongoni mwa Watanzania, kujenga mifarafakano.

"Wakaenda mbali zadi wakaanza kuzusha jambo ambalo wanataka kuifanya ajenda, wanasema nchi ina Rais ambaye ni Mzanzibari na anaihujumu Bara, lakini ajenda hiyo imeshindwa."

Ameongeza CHADEMA wanazungumza kuhusu Rais Samia ni Mzanzibar, hana huruma na Bara, hana jema analofanya kwa Bara, hana msaada.

“Wanataka kumtenganisha Rais na Watanzania, nani amekataa kwamba Rais Samia sio Mzanzibari. Ni Mzanzibari na ametokana na Katiba ambayo inaeleza mgombea urais akitoka Zanzibar basi mgombea mwenza anatoka upande wa pili…

“Ndivyo tulivyokubaliana na huyu ni mgombea mwenza ana nafasi sawa na mgombea urais. Ikitokea mgombea mwenza hayuko uchaguzi unaahirishwa. Mwaka 2005 uchaguzi uliahirishwa kwa sababu mgombea mwenza wa CHADEMA alifariki dunia.

“Halafu leo wanakejeli kiongozi kutoka Zanzibar, wametafuta namna ya kushughulika na Rais (Dk. Samia) lakini wakiangalia barabara zinajengwa, bwawa la mwalimu Nyerere limefika pazuri, ujenzi wa mji wa Dodoma unaendelea kwa kasi.

“Reli ya mwendo kasi sasa imefika Dodoma na ujenzi unaendelea sasa wanakosa hoja wanakuja na maneno ya kuzusha kwamba Rais hafai kwa sababu anatoka Zanzibar. Rais Samia ni Rais wa katiba amechukua uongozi baada ya Rais Dk. John Magufuli kufariki dunia,” alisema.

Ameongeza kwamba “Rais Samia alikuwa Mgombea Mwenza akawa Makamu wa Rais, na awamu ya pili Magufuli akamteua tena lakini oooh… huyo Mzanzibar ili watu baadae polepole waanze kusema tunatawaliwa na Mzanzibari.”

Amewaomba Watanzania kupuuza uzushi huo na kushauri wasimame na Rais Samia kwani anafanya kazi nzuri.

"Tangu awamu mbalimbali zilizopita kuna sera iliyoanza baada ya Mzee Mwinyi kuchukua nchi kwa kuanzisha sera ya sekta binafsi kushiriki kukuza uchumi.

“CHADEMA wanasema Rais Samia anauza kila kitu, kauza nini?. Awamu ya Tatu Rais mstaafu Benjamin Mkapa alibinafsisha mashirika zaidi ya 200 kwani alikuwa Mzanzibar?

“Wakati TICS wanapewa bandari ya Dar es Salaam nchi haikuuzwa, lakini baada ya kupewa DP World nchi inauzwa. Hivi mnaamini kweli Rais anaweza kukaa na kufanya jambo ambalo halina nia njema na nchi yetu.

“Rais haamui peke yake kuna vyombo ambavyo vinakaa na kuangalia mambo na kisha vinamshauri Rais. Kataeni juhudi zinazofanyika za kujenga chuki dhidi ya Rais. Kuna wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilikabidhiwa kwa RITES (kampuni) kutoka India? Alikabidhi Rais Samia?”

Kinana amesema hayo mambo yanafanyika kwa malengo na hasa kuleta tija na ufanisi, hivyo Watanzania wasikubali kusikiliza hoja rejareja, hoja za msimu.

Pia amesema Rais Samia ambaye wanamsema ndiye ameleta uhuru wa kusema, kushutumu, kuandamana. Mikutano ya hadhara wanaweza kusema iko katika Katiba lakini huko nyuma wakati wananyimwa kwani haikuwepo kwenye Katiba?.

“Katiba ilikuwepo, uhuru ulikuwepo lakini walikatazwa kwenda barabarani. Amekuja Rais muungwana ameondoa kifungo. Akisema kuanzia leo hakuna maandamano, watafanya? Wanamkejeli na kumtuhumu Rais amekaa kimya.

“Waamuzi ni wao. Wana CCM dawa yao kwenye sanduku la kura, wenzetu wanatafuta nguvu katika sanduku la kura. Watanzania hawapendi kejeli. Nina uhakika adhabu watakayopata watajutia.

Kuhusu hoja ya Katiba, sheria mpya ya uchaguzi na muungano Kinana amesema kwamba ukisikiliza kwa makini utabaini wanataka kuleta mfarakano kati ya bara na Zanzibar.

“Wamekuwa wakizunguka na ajenda ya kuligawa taifa katika majimbo, hii ni sera ambayo wamekuwa nayo kwa muda. Msimamo wa CCM Watanzania tusikubali kugawanywa kwa namna yoyote,” amesema Kinana.

Akizungumzia Katiba mpya ,Kinana amesema kulifanyika mazungumzo kwa mwaka mzima baina ya CHADEMA na CCM na kwa maoni yao walisema si ajenda yao ya sasa, lakini Kamati Kuu baada ya ushawishi wakakubali.

“Kimsingi Katiba hatukatai lakini wenzetu wanataka Katiba ipatikane leo, katika kile kikao walituambia tunaelewa Katiba hii haitakuwa leo lakini tunawasihi mkubali uwepo wa Katiba, tukatoa tamko na muda mwafaka tutakubaliana.

“Wenzetu wanasema wanataka Katiba sasa, katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam Rais alisema Katiba mpya haiwezi kuwa ya vyama vya siasa peke yao,”amesema.

Ameongeza Katiba ya sasa imefanyiwa marekebisho mara 14 na sababu ukiangalia sio mambo yaliyohusu wananchi bali ni Siasa, madaraka na uchaguzi.








Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) inaendelea na kazi ya utoaji mafunzo kwa Walimu Wakuu wa shule za msingi za Serikali na zisizo za Serikali nchini kwa lengo la kuwajengea uelewa wa namna bora ya kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Mtaala wa Elimu ya Awali na Msingi wa Mwaka 2023.

Akizungumzia kuhusu mafunzo Mkurugenzi Mkuu wa TET , Dkt. Aneth Komba amesema kuwa mafunzo hayo yatafanyika Kwa walimu Wakuu wote katika Halmashauri 184 kuanzia leo tarehe 5/5/2024 hadi 12/6/2024 kwa awamu tofauti ambapo katika awamu ya kwanza, mafunzo yatafanyika katika Halmshauri za Mkoa wa Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Kagera Kigoma, Geita na Tabora.

“Tunaendelea na mafunzo na awamu hii ni ya walimu wakuu wote nchi nzima ambapo tufanafaya mafunzo kwa awamu tofauti tofauti”amesema Dkt.Komba.

Aidha, Dkt. Komba ameeleza kuwa mafunzo ni ya muhimu kwakuwa walimu Wakuu wataweza kusimamia na kufuatilia utekelezaji wake na kuweza kutoa msaada (Mentorship and Support) kwa walimu wengine masomo pale inapohitajika.

Wawezeshaji na waratibu wa mafunzo hayo ni kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, OR-TAMISEMI na TET,huku akiishukuru Serikali ya Awamu ya sita inayoongzwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha mafunzo hayo kufanyika kwa walimu wote nchini.








Top News